Dec 07, 2023 06:15 UTC
  • Afisa wa Yemen: Bahari Nyekundu ni marufuku kwa usafiri wa meli za utawala wa Kizayuni

Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Yemen amesema, Bahari Nyekundu kutoka Ghuba ya Aqaba hadi Bab al-Mandab ni marufuku kwa safari za aina yoyote za meli za utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa tovuti ya mtandao wa Al-Masirah, Mohammed Nasser Al-Atafi, Waziri wa Ulinzi wa Yemen amesema, isipokuwa utawala wa Kizayuni, Bahari Nyekundu (Bahari ya Sham) ni eneo salama kwa usafiri na biashara za nchi zote za dunia.

Kauli hiyo ya Waziri wa Ulinzi wa Yemen imetolewa saa chache baada ya Msemaji wa Jeshi la Yemen Yahya Saree kutangaza habari ya kurushwa makombora kadhaa ya balistiki katika mji wa Eilat ulioko kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na ikiwa ni operesheni ya kumi na mbili ya jeshi la Yemen katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni.

Makombora ya Yemen

Yahya Saree amesema: Kitengo cha makombora cha Yemen kimerusha makombora ya balistiki mfululizo katika maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika eneo la Um al-Rasrash huko Eilat, kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Afisa huyo wa Yemen amesema: 'Tutaendeleza oparesheni zetu za kijeshi dhidi ya adui Israel, pamoja na  kuzuia harakati za meli zake katika Bahari ya Arabia na Bahari Nyekundu kwa ajili ya kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina, hadi kukomeshwa mashambulizi dhidi ya ndugu zetu huko Gaza.'

Jeshi la Yemen hapo awali lilitangaza kulenga meli yoyote ya Israel ikiwa ni katika  kukabiliana na mashambulizi ya kijeshi ya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, katika Ukanda wa Gaza.

Tags