Dec 07, 2023 07:06 UTC
  • Jeshi la Kizayuni limeua kwa halaiki jamaa 22 wa familia ya ripota wa Aljazeera

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imelaani mauaji ya familia ya mmoja wa waandishi wake wa habari katika mashambulizi yaliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel huko Gaza.

Katika shambulio lililofanywa na utawala wa Kizayuni katika kambi ya Jabalia iliyoko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, watu 22, akiwemo baba na kaka kadhaa wa ripota wa Al Jazeera Momin Al-Sharafi wameuawa shahidi pamoja na watoto wao.

Kwa mujibu wa Al-Jazeera, ripota wa chaneli hiyo ya televisheni Momin Al-Sharafi ametaka jeshi la Kizayuni lifunguliwe mashtaka kwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari na raia wa Gaza.

Baadhi ya waandishi wa habari waliouawa shahidi Gaza

Al-Sharafi ameongeza kuwa: chaneli hiyo ya habari itachukua hatua zinazohitajika kisheria katika taasisi husika ili kuwafuatilia na kuwafungulia mashtaka maafisa wa Kizayuni waliohusika na jinai hiyo ya kutisha.

Akisimulia jinai hiyo waliyofanyiwa watu wa familia yake, ripota huyo wa Al Jazeera amesema: askari wa utawala wa Kizayuni walidondosha pipa la mada za miripuko juu ya nyumba waliyokuwemo ndani yake watu wa familia yake.

Mbali na familia za waandishi wa habari, utawala dhalimu wa Kizayuni umeshaua pia makumi ya waandishi wa habari tangu ulipoanzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni, wanahabari wasiopungua 73 wameuawa shahidi ndani ya kipindi cha siku 57 za vita vya Gaza.

Wakati huohuo Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza katika ripoti yake kuwa zaidi ya watu 16,000 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, na takribani watu 41,000 wamejeruhiwa huku wengine 1,000 wakiwa hawajulikani waliko.../

Tags