Dec 08, 2023 03:19 UTC
  • Rais wa Iran akiwa safarini Russia asisitiza kusitishwa jinai za Israel dhidi ya Gaza

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kusitishwa mara moja jinai za Israel za "mauaji ya kimbari" dhidi ya Wapalestina Ukanda wa Gaza.

Rais wa Iran ameyasema hayo alipokutana na mwenzake wa Russia  Vladimir Putin mjini Moscow siku ya Alhamisi ambapo mazungumzo yao yalihusu uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza na kuimarisha uhusiano kati ya Tehran na Moscow.

Rais wa Iran aliongeza kuwa: "Gaza ni ardhi ambayo mtoto huuawa shahidi kila baada ya dakika kumi, kwa hivyo ni muhimu kusitisha udondoshaji huu wa mabomu haraka iwezekanavyo na kutafuta suluhu ya haraka." Aidha aliongeza kuwa "kinachotokea Palestina ni mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu”.

Aliendelea kwa kuongeza kwamba: "Uhalifu wa utawala wa Kizayuni huko Gaza unaungwa mkono na Marekani na nchi za Magharibi, na inasikitisha kwamba mashirika ya kimataifa yanayodai kutetea haki za binadamu yamepoteza uwezo wao wa utendaji kazi."

Rais wa alisema, "Kinachowatesa wanadamu leo ni mfumo upande mmoja na mfumo usio wa haki wa kimataifa, na dhihirisho lake linaweza kuonekana Gaza."

Putin alimpokea Raisi siku moja baada ya safari yake  Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, ambako alizungumzia Gaza na Ukraine na juhudi za Russia na OPEC za kuongeza bei ya mafuta.

Mkutano wa Marais Raisi wa Iran na Putin wa Russia

Rais wa Iran aligusia uhusiano imara kati ya Russia na Iran, akisema bila shaka kuna nafasi ya kuuendeleza zaidi.  Rais Putin alibainisha furaha yake kubwa ya kuwa mwenyeji wa Rais wa Iran jijini Moscow  na kuongeza kwamba: "Ni muhimu kwamba leo tubadilishane mawazo kuhusu masuala ya kikanda, hasa hali ya Palestina."

Vile vile amegusia kukua kwa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, akisema chini ya mpango wa sasa, kutiwa saini makubaliano ya biashara huria kati ya Iran na ujumbe wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia ni ajenda ya Russia.

Rais Putin aidha alisema: "Uhusiano kati ya nchi hizi mbili unaendelea kwa kasi. Nitashukuru kama ungeweza kufikisha salamu zetu za heri kwa Kiongozi Muadhamu [Ayatullah Seyyed Ali Khamenei], kwa sababu anaunga mkono mahusiano yetu.”

 

Tags