Dec 08, 2023 15:22 UTC
  •  Hamas yawaomba wapigania uhuru duniani kushiriki maandamano ya mshikamano na Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imezitolea wito nchi za Kiarabu, Kiislamu na wapigania uhuru kote duniani kuandamana tangu leo ili kutangaza mshikamano na kuwa pamoja na wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza.

Harakati ya Hamas ya Palestina imezitaka nchi za Kiarabu, Kiislamu na mataifa huru ya dunia wakiwemo wanazuoni wa kidini, watu wenye ushawishi mkubwa, taasisi na jumuiya zenye taathira kutangaza mshikamano na watu wa Gaza na kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni kuanzia leo ili kuwezesha kufikishwa misaada ya kibinadamu na vifaa vya matibabu katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, na pia kusimamisha mashambulizi ya utawala huo. 

Hamas pia imewaomba wapigania uhuru na wanaharakati na wapigania ukombozi kote duniani kuendeleza shughuli zao za kiraia za kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina, lengo likiwa ni kukomesha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na mauaji ya kizazi dhidi ya raia wa Palestina wakiwemo watoto na wanawake.  

Mauaji ya watoto wa Gaza yanayofanywa na utawala haramu wa Israel 

Mwishoni mwa taarifa yake, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeeleza kuwa: "Tuungane sote leo Ijumaa na katika siku zijazo, na tuonyeshe mshikamano wetu na watu wa Gaza na Palestina na kupinga jinai za wavamizi hadi kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu.