Feb 23, 2024 03:29 UTC
  • Vikosi vya Yemen vyashambulia bandari ya Israel, meli ya mizigo ya Uingereza, na meli ya kivita ya Marekani

Vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza kutekeleza operesheni tatu za kijeshi ambapo ya kwanza imelenga bandari ya Eilat inayokaliwa na Israel ya pili meli ya mizigo ya Uingereza katika Ghuba ya Aden na ya tatu meli ya kivita ya Marekani katika Bahari Nyekundu kwa kutumia makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani.

Taarifa iliyotolewa Alhamisi ilisema operesheni hizo zilianzishwa "kuunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina, na kama sehemu ya jibu kwa uchokozi wa  Marekan na Uingereza dhidi ya nchi yetu".

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: "Wakati wa operesheni ya kwanza, kikosi cha makombora na kikosi cha anga cha Wanajeshi wa Yemeni kilivurumisha idadi kubwa ya makombora ya balestiki na kutumia ndege zisizo na rubani kulenga maeneo mbali mbali ya adui Mzayuni katika eneo la Umm al-Rashrash (Eilat) kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu."

Aidha taarifa hiyo imebaini kuwa: "Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu operesheni ya pili ilifanyika katika Ghuba ya Aden, ambapo jeshi la wanamaji la Yemen limelenga meli ya mizingio ya  Uingereza (ISLANDER) katika Ghuba ya Aden kwa makombora ya jeshi la majini na kusababisha moto katika meli hiyo."

Halikadhalika taarifa hiyo imesema: "Operesheni ya tatu ilihusisha kulenga meli ya kivita ya Kimarekani katika Bahari Nyekundu kwa ndege za kivita zisizo na rubani."

Mapema Alhamisi, jeshi la Uingereza lilitangaza kuwa meli inayomilikiwa na kampuni ya Uingereza ilichomwa moto katika pwani ya kusini mwa Yemen baada ya kushambuliwa kwa kombora katika Ghuba ya Aden.

Data ya ufuatiliaji wa meli ilibainisha kuwa meli hiyo iliyoteketezwa ni meli ya mizigo yenye bendera ya Palau iitwayo Islander.

Hayo yanajiri wakati ambao kiongozi wa Harakati ya Ansarullah Abdul-Malik al-Houthi alitangaza  Alhamisi kwamba  Jeshi la Yemen limeanza kutumia 'silaha za nyambizi' dhidi ya meli zinazomilikiwa na Israel au zinazohusiana na utawala huo.

Yemen imetuma ilani rasmi kwa mashirika ya bima duniani na kutangaza kuwa  meli ambazo zote zinamilikiwa na watu binafsi  wanaohusishwa na Israel au mashirika ya utawala wa Israel; Meli zenye bendera ya Israel, au zile zinazomilikiwa na watu au mashirika ya Marekani au Uingereza, au kusafiri chini ya bendera za Marekani au Uingereza, zimepigwa marufuku kupita Bahari Nyekundu, Ghuba ya Aden na Bahari ya Arabia.

Operesheni hizo za kijeshi za Yemen ni katika kuwatetea Wapalestina ambao wanakabiliwa na hujuma ya utawala haramu wa Israel kwa himaya ya Marekani na Uingereza.