Feb 23, 2024 03:30 UTC
  • HAMAS: Kimbunga cha al-Aqsa kimevuruga njama za US katika eneo

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa iliyofanywa na makundi ya muqawama ya Ukanda wa Gaza ilisitisha njama za Marekani za eti kulifinyanga eneo la Asia Magharibi na mustakabali wake.

Osama Hamdan, Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen na kuongeza kuwa, operesheni hiyo ya kishujaa ya wanamuqawama imevuruga kikamilifu mahesabu ya Marekani katika eneo.

Ameeleza bayana kuwa, "Utawala wa Marekani haujawahi kuwa mpatanishi au msuluhishi, bali daima umekuwa mshirika wa Israel, na moja ya matokeo muhimu ya  Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni kwamba (operesheni hiyo) ilizima mipango ya Marekani kwa eneo hili na muskatabali wake; mipango iliyokuwa ifanyike kwa maslahi ya Washington na utawala ghasibu wa Israel."

Hamdan amebainisha kuwa, muqawama umesambaratisha ndoto za Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, ambaye amesalia katika njozi juu ya utekelezaji wa mradi wa kiaidiolojia wa Uzayuni.

Osama Hamdan, Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon

Amesisitiza kuwa, madhali utawala haramu wa Israel unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, makundi ya muqawama hayana chaguo jingine isipokuwa kuwapa himaya wananchi hao madhulumu na wasio na ulinzi wa eneo hilo.

Hamdan amesema njia pekee ya kupatika utulivu kwenye ukanda huu mzima ni kusimamishwa vita, kukomeshwa uvamizi na kuundwa nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Quds Tukufu.

Kadhalika kiongozi huyo wa ngazi za juu wa HAMAS ameongeza kuwa, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza imezidi kuwa mbaya na kuna udharura wa kupelekwa haraka dawa na chakula kwa wakazi wote wa ukanda huo.

Tags