Feb 28, 2024 02:52 UTC
  • Yemen: Mashambulizi katika Bahari ya Sham yatakoma pale tu Israel itakapositisha vita Gaza

Msemaji wa Harakati ya Ansarullah inayotawala Yemen amesema mashambulizi ya nchi hiyo ya Kiarabu dhidi ya meli za maadui katika Bahari ya Sham yatakoma tu baada ya utawala wa Israel kuhitimisha vita na mzingiro wake dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Mohammed Abdul-Salam, ambaye pia ni mjumbe mkuu wa mazungumzo katika Harakati ya Ansarullah aliyasema hayo Jumanne, wakati jeshi la Yemen likiendelea kushambulia meli zenye uhusiano na utawala haramu wa Israel, pamoja na meli za Marekani na Uingereza, zinazopita katika bahari hiyo.

Alipoulizwa iwapo oparesheni za jeshi la Yemen katika Bahari ya Sham zitaisha iwapo kutakuwa na usitishaji vita kati ya utawala wa Israel na harakati ya muqawama ya Hamas yenye makao yake makuu Gaza, Abdul-Salam alisema kuwa hali hiyo itaangaliwa upya iwapo Israel itamaliza mzingiro wake dhidi ya Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia eneo hilo la Palestina.

Wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya Israel tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita vikali dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kutekeleza operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya walowezi wa Israel na vikosi vya kijeshi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimesema havitakomesha mashambulizi ya kulipiza kisasi hadi mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Israel huko Gaza, ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 30,000 na wengine 70,000 kujeruhiwa, yatakapomalizika kabisa.

Mashambulizi Bahari ya Sham yamelazimisha baadhi ya makampuni makubwa ya meli za biashara na mafuta kusimamisha usafiri kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya baharini.