Mar 02, 2024 03:07 UTC
  • Ben-Gvir awapongeza wanajeshi wa Israel walioua zaidi ya Wapalestina 100 Ghaza, US yaizuia UN isitoe tamko

Waziri wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mwenye misimamo mikali ya chuki amewapongeza wanajeshi wa utawala huo walioua zaidi ya Wapalestina 100 waliokuwa wakisubiri misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza uliowekewa mzingiro.

Itamar Ben-Gvir, anayeongoza wizara eti ya usalama wa taifa ya Israel amesema: "lazima tuwaunge mkono kikamilifu wapiganaji wetu mashujaa wanaoendesha oparesheni huko Ghaza, ambao walichukua hatua barabara dhidi ya genge la watu wa Ghaza ambao walijaribu kuwadhuru".

Ben-Gvir, vilevile ametilia mkazo tena takwa lake la kuzuia kuingizwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza, akidai kuwa "inahatarisha" wanajeshi wa Israel.

Mapema siku ya Alkhamisi, vikosi vya Israel viliwafyatulia risasi Wapalestina waliokuwa wakisubiri msaada wa kibinadamu karibu na mzunguko wa al-Nabulsi katika mji wa Ghaza, na kuua watu wasiopungua 112 na kujeruhi wengine 760.

Mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na wanajeshi katili wa Israel yamelaaniwa na kushutumiwa vikali na mataifa na jumuiya tofauti za kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amelaani vikali "shambulio hilo la kinyama", na kubainisha kwamba "aibu ya kuunga mkono na kunyamazia kimya mauaji halaiki na ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni itadhihirika kwenye mapaji ya nyuso za mabingwa bandia wa haki za binadamu wa ndani ya Marekani na Ulaya."

Hayo yanajiri huku shirika la habari la Anadolu likiripoti kuwa, taarifa kutoka ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinaeleza kwamba Marekani imelizuia baraza hilo kutoka tamko kuhusiana na shambulio la jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina waliokuwa wakingojea kupatiwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza.

Kwa mujibu wa Anadolu, wakati wa kikao cha Baraza la Usalama kilichofanyika makao makuu ya UN mjini New York, nchi wanachama zilijadili kutoa tamko kuhusiana na shambulio hilo, lakini kikao hicho kilimalizika bila kutolewa taarifa yoyote.

Kulingana na taarifa lilizopokea shirika la habari la Anadolu, rasimu ya azimio lililokuwa na matamshi ya ukosoaji dhidi ya Israel ilishindwa kupata idhini ya Ujumbe wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.../

 

Tags