Mar 02, 2024 03:07 UTC
  • Baada ya mazungumzo ya Moscow, mirengo ya Palestina yaapa kuungana pamoja dhidi ya Israel

Makundi ya Palestina ikiwemo Hamas na Fat-h yamesema yatafuata "umoja wa kivitendo" katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya wawakilishi wao kukutana katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Russia mjini Moscow.

Taarifa ya jana Ijumaa iliyotolewa makundi ya Wapalestina yaliyowakilishwa mjini Moscow ilisema, kutakuwa na "mazungumzo yajayo" ili kuwaweka chini ya bendera ya Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO).
 
Mkutano wa Moscow uliofanyika siku ya Alkhamisi ulizileta pamoja harakati za Hamas, Jihadul-Islami, Fat-h na makundi mengine ya Wapalestina kwa ajili ya mazungumzo ya kujadili vita vya kinyama vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Ghaza na hali ya baadaye ya kipindi cha baada ya vita.
 
Mkutano huo umefanyika kufuati kujiuzulu Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ambayo inaongozwa na Fat-h na yenye makao yake makuu mjini Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Mohammad Shtayyeh

Waziri Mkuu aliyejiuzuulu Mohammad Shtayyeh alitoa wito wa kuwepo kwa maelewano ndani ya Palestina alipokuwa akitangaza uamuzi wake huo, na baadhi ya wachambuzi walisema matukio hayo yanaweza kufungua njia ya kuundwa serikali ya wanateknokrati ambayo itakayokuja kufanya kazi baada ya vita katika Ukingo wa Magharibi na pia Ukanda wa Ghaza unaoongozwa na serikali ya Hamas.

 
Viongozi wa nchi za Kiarabu na wa madola ya Magharibi wamekuwa wakishinikiza kufanyika mageuzi katika serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina huku wakijadili uwezekano wa kuanzishwa juhudi za ujenzi mpya katika eneo la Ghaza.
 
Taarifa ya mirengo ya Palestina imebainisha kuwa, mazungumzo ya Alkhamisi "ya kujenga" yalishuhudia kufikiwa mwafaka na makubaliano juu ya masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na haja ya kuondoka majeshi ya Israel huko Ghaza na kuundwa taifa la Palestina.../

 

Tags