Mar 03, 2024 12:23 UTC
  • Shehbaz Sharif
    Shehbaz Sharif

Shehbaz Sharif ameteuliwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan kwa mara ya pili, wiki tatu baada ya uchaguzi wenye utata uliopelekea kuundwa kwa serikali ya mseto.

Bunge jipya la Kitaifa la Pakistan, kama liitwalo baraza la chini la bunge, lilimchagua Sharif jana Jumapili kuwa waziri mkuu kwa kura 201, na kuongoza muungano ulioyumba ambao umewafungia nje wafuasi wa kiongozi wa upinzani, Imran Khan aliyefungwa jela.

Spika mpya aliyeteuliwa wa Bunge la Kitaifa, Sardar Ayaz Sadiq anesema Shehbaz Sharif ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Pakistan,"

Omar Ayub Khan alikuwa mgombea aliyeungwa mkono wa Wabunge waliomuunga mkono Khan, na kupata jumla ya kura 92 katika jitihada zake dhidi ya Sharif.

Katika Bunge la kitaifa la Pakistan, linalojumuisha wajumbe 336, 266 wanachaguliwa kupitia kura ya moja kwa moja, huku 70 wakiteuliwa. Miongoni mwa wajumbe walioteuliwa, viti 60 vimetengwa kwa ajili ya wanawake na 10 kwa wawakilishi wa dini za waliowachache

Chama cha kisiasa au muungano unahitaji viti 169 katika bunge la kitaifa ili kuchukua mamlaka, huku uteuzi wa wateule huamuliwa na utendaji wa uchaguzi wa kila chama cha kisiasa.

Imran Khan

Sharif, 72, ni kaka mdogo wa Waziri Mkuu wa mara tatu Nawaz Sharif, ambaye aliongoza kampeni za uchaguzi za chama cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N).

Wagombea wanaoungwa mkono na Khan walipata viti vingi zaidi lakini PML-N na Pakistan Peoples Party zilikubali kuunda serikali ya mseto, ambayo ilimwezesha Shahbaz Sharif kuchaguliwa kuwa waziri mkuu huku kaka yake akiondoka.

Sharif alihudumu kama waziri mkuu hadi Agosti mwaka jana wakati Bunge la Kitaifa lilipovunjwa ili kufungua njia kwa serikali ya mpito yenye jukumu la kusimamia uchaguzi wa kitaifa.

Pakistani ilifanya uchaguzi mnamo Februari 8 huku kukiwa na utata. Matokeo yaliyocheleweshwa yalizua shutuma za wizi wa kura na udanganyifu katika uchaguzi.

Katika historia ya miaka 77 ya Pakistan, hakuna waziri mkuu ambaye amefaulu kuhudumu kwa muhula mzima wa miaka mitano, kutokana na ushawishi mkubwa wa kisiasa unaotumiwa na jeshi.