Apr 13, 2024 10:13 UTC
  • Hizbullah yashambulia maeneo ya jeshi la Israel kwa makumi ya maroketi

Harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah imetekeleza operesheni kadhaa dhidi ya maeneo ya kijeshi ya utawala wa Israel na kuonyesha uungaji mkono wake usioyumba kwa Wapalestina wakati wa vita vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza.

Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon ya lugha ya Kiarabu, imenukuu taarifa ya Hizbullah ikisema harakati hiyo imevurumisha mizinga na makombora katika eneo la Malikiyah na kusababisha majeraha kwa vikosi vya utawala ghasibu wa Israel.

Wapiganaji wa Hizbullah pia wameshambulia eneo la al-Marj kwa safu ya makombora, na kupiga kwa usahihi maeneo yaliyolengwa.

Wapiganaji wa Hizbullah pia wameshambulia maeneo ya Ruwaisat al-Alam na al-Samaqa katika kijiji cha Kfarchouba nchini Lebanon kwa mizinga na makombora.

Hali kadhalika wameshambulia kambi ya nje ya Karantina Hill kwa roketi kadhaa na kufanya shambulio jingine la ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya Israeli huko Ramot Naftali Moshav.

Utawala wa Israel umekuwa ukishambulia mara kwa mara eneo la kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari  dhidi ya Gaza na kusababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 33,634 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Katika kulipiza kisasi, Hizbullah imekuwa ikitekeleza kwa mafanikio mashambulizi ya maroketi, makombora na mizinga karibu kila siku dhidi ya Israel.