Dec 16, 2018 11:08 UTC
  • Kuakisiwa gwaride la vikosi vya muqawama vya Palestina mjini Ghaza + Picha

Bridegi za Izuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS jana Jumamosi zilifanya gwaride kubwa lililofana la kijeshi katika Ukanda wa Ghaza.

Katika maonesho hayo ya nguvu za kijeshi, HAMAS ilionesha silaha zake mpya za kisasa kabisa yakiwemo makombora na maroketi ya kila namna. Ujumbe wa gwaride hilo ambalo ni sawa na kutanua misuli ya kijeshi muqawama wa Palestina mbele ya utawala pandikizi wa Kizayuni ni kwamba kama Israel itaendelea na chokochoko zake, basi itapata pigo kubwa isilolitarajia kutoka kwa muqawama wa Palestina.

Gwaride hilo la kijeshi limefanyika sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 31 wa tangu kuasisiwa harakati ya Kiislamu ya HAMAS. Harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu iliasisiwa na Sheikh Ahmad Yasin katikati ya mwezi Disemba 1987 sambamba na kuanza Intifadha ya Kwanza ya Wapalestina. Matukio ya Palestina yanaonesha kuwa, licha ya kuongezeka kupindukia ukandamizaji na ukatili wa utawala wa Kizayuni wenye lengo la kuwadhoofisha na hatimaye kuwamaliza nguvu kabisa wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina, lakini uwezo wa kujihami makundi ya muqawama ya Palestina likiwemo la Hamas unazidi kuwa mkubwa licha ya kwamba Israel imeuzingira kila upande Ukanda wa Ghaza kwa miaka mingi sasa. Nguvu hizo za wanamapambano wa Kiislamu wa Palestina, bila ya shaka yoyote zinautia kiwewe kikubwa utawala wa Kizayuni. Hasa kwa kuzingatia kuwa, lengo kuu la Israel ni kuuangamiza muqawama na kuwapoka silaha wanamapambano wa Palestina katika vita unavyovianzisha mara kwa mara Ukanda wa Ghaza, lakini njama hizo pia zimefeli kama zilivyofeli njama nyingine zote za Wazayuni.

Sehemu ya silaha za kisasa za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Hatua ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ya kuonesha uwezo wake mkubwa wa kijeshi na kuungwa mkono kikamilifu na wananchi wa Ghaza, si jambo linalowapendeza hata kidogo Wazayuni. Mafanikio ya muqawama wa Palestina ya kutoa kipigo kwa utawala wa Kizayuni na hivyo Israel kulazimika kusimamisha mara moja uvamizi wake baada ya siku mbili tu za kuivamia Ghaza mwezi Novemba mwaka huu, yameonesha upeo wa kujizatiti wanamapambano wa Kiislamu huko Ghaza katika kukabiliana na ukatili wa Wazayuni. Hivi sasa mlingano wa nguvu katika eneo hilo umebadilika, na zile zama za Israel kushambulia Ukanda wa Ghaza na kuondoka salama usalimini zimeisha. Kulazimika utawala wa Kizayuni kukomesha uvamizi wake wa wa pande zote wa kijeshi huko Ghaza siku mbili tu baada ya kuuanzisha kutokana na majibu makali ya wanamuqawama wa Palestina ni ushahidi mwingine wa udhaifu wa Israel na woga walio nao Wazayuni katika kukabiliana na wanamapambano wa Kiislamu. Kusema kweli, kushindwa mtawalia utawala wa Kizayuni mbele ya muqawama wa wananchi wa Palestina katika miaka ya hivi karibuni kumebatilisha propaganda chapwa za utawala huo uliokuwa unajilabu kuwa eti haushindiki. Vile vile ushindi wa mara kwa mara wa kambi ya muqawama dhidi ya Wazayuni umezidi kuwatia moyo Wapalestina na kuwadhoovisha Wazayuni maghasibu kiasi kwamba Wapalestina wanasema kuwa, ushindi huo ni utangulizi wa kukombolewa ardhi zote za Palestina kutoka kwenye makucha katili ya Israel. 

Sehemu ya gwaride la kuonesha nguvu za Hamas Ukanda wa Ghaza Palestina

 

Kwa hakika hatua ya Wapalestina ya kuonesha nguvu zao za kijeshi huko Ghaza ni ushahidi wa kufeli Israel kudhoofisha nguvu za Wapalestina kupitia kuyazingira kila upande maeneo yao. Itakumbukwa kuwa, kuanzia mwaka 2007 hadi hivi sasa, utawala wa Kizayuni umeshadidisha mashinikizo yake dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuufungia njia zote za kuingia na kutoka Ukanda wa Ghaza ili kuwalazimisha wakazi wa ukanda huo waachane na muqawama na waipigie magoti Israel. Lakini jinai hizo za utawala wa Kizayuni si tu zimefeli kufikia lengo hilo, bali zimewafanya Wapalestina wapate moyo zaidi ya kujitegemea na kusimama imara kukabiliana na wavamizi wa ardhi zao na hivi sasa Intifadha ya kutumia silaha imeenea sehemu mbalimbali za Palestina hata katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, awamu hii mpya ya mapambano ya wananchi wa Palestina haitokuwa na matunda mengine isipokuwa tu kuzidi kupata vipigo utawala vamizi wa Kizayuni.

 

Tags