Jan 28, 2023 11:50 UTC
  • Wapalestina wapongeza operesheni ya al-Quds, wasema ni kulipiza kisasi kwa mauaji ya Jenin

Makundi ya muqawama na mapambano ya ukombozi wa Palestina yamepongeza operesheni ya kulipiza kisasi karibu na sinagogi katika makazi haramu ya walowezi wa Kizayuni kwenye eneo la al- Quds (Jerusalem) Mashariki linalokaliwa kwa mabavu na Israel, na kueleza kuwa oparesheni hiyo ni 'jibu la moja kwa moja' kwa uvamizi mbaya zaidi wa kijeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi

Duru za habari zimeripoti usiku wa kuamkia leo kuwa, Wazayuni saba waliangamizwa kwa kupigwa risasi kaskazini mwa mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu.

Vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel vimeripoti kuwa, walowezi saba wameangamizwa kufuatia ufyatuaji risasi uliotokea katika eneo la An-Nabiyyu-Yaaqub, lililoko kaskazini mwa al-Quds. Vyanzo vya Kizayuni vimetangaza kuwa watu 12 walijeruhiwa pia katika shambulio hilo la ufyatuaji risasi.

Wazayuni hao saba wameangamizwa baada ya shambulizi la siku ya Alkhamisi la wanajeshi katili wa Israel katika kambi ya wakimbizi Wapalestina huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambako waliwaua shahidi Wapalestina kumi na kuwajeruhi wengine 20.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema katika taarifa yake kwamba shambulio la Ijumaa lilikuwa "jibu la kawaida kwa mauaji ya Jenin, kuvunjiwa heshima eneo lililobarikiwa la Msikiti wa al-Aqsa, na kukithiri jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Hamas imesema oparehseni hiyo inatoa ujumbe kwa utawala ghasibu wa Israel kwamba nguvu za Wapalestina haziwezi kudhoofishwa.

Hali baada ya jeshi katili la Israel kushambulia kambi ya Jenin

Harakati ya muqawama ya Jihad Islami pia imepongeza oparesheni ya al-Quds Mashariki, ikisema katika taarifa yake kwamba "ilikuja kwa wakati na mahali mwafaka kulipiza kisasi cha damu ya mashahidi katika kambi ya Jenin na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Ilikuwa jibu la asili na halali kwa uhalifu wa utawala vamizi wa Israel."

Aidha Harakati ya Wananchi kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) imetoa pongezi kwa wapiganaji wa muqawama wa kishujaa, na kusisitiza kwamba operesheni ya al-Quds Mashariki ni kielelezo cha irada ya taifa la Palestina katika kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel.

Nayo Kamati ya Wananchi ya Muqawama (PRC) imesema kuwa operesheni iliyofanyika katika makazi haramu ya Nabii Yacov ni jibu la kivitendo na mwafaka kwa jinai za utawala wa Israel katika kambi ya Jenin na kwengineko katika ardhi za Palestina.

Kwa upande wake Chama cha Demokrasia cha Ukombozi wa Palestina kimesema katika taarifa yake kwamba, operesheni ya kishujaa huko al-Quds Mashariki ni mwanzo wa awamu mpya ya muqawama wa wananchi dhidi ya Israel.

Tags