Jan 29, 2023 02:35 UTC
  • Kuendelea ukandamizaji wa Aal Khalifa dhidi ya wafungwa wa kisiasa katika kukaribia mwaka wa 12 wa mapambano ya wananchi

Katika kukaribia maadhimisho ya kutimia mwaka wa 12 wa mapambano ya wananchi wa Bahrain, utawala wa ukoo wa Aal Khalifa nchini Bahrain unawazuia wafungwa wa kisiasa nchini humo kuwasiliana na kuoana na familia zao katika fremu ya sera zake za ukandamizaji na kuwawekea mbinyo na vizingiti mbalimbali wafungwa wa kisiasa na wapinzani nchini humo.

Mwaka 2011 Bahrain iligubikwa na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa kidikteta wa nchi hiyo kama ilivyoshuhudiwa katika nchi nyingine kadhaa za Kiarabu. Kinyume na nchi kama Tunisia, Misri na Libya ambako vuguvugu la mapambano ya wananchi lilimalizika kwa njia mbalimbali, huko Bahrain wananchi wangali wanaendeleza mapambano dhidi ya utawala kandamizi wa ukoo wa Aal Khalifa. Mapambano ya wananchi wa Bahrain yamekuwa ya amani kikamilifu na bado yanaendelea katika mkondo huo baada ya kupita miaka 12 sasa. Mkabala wake, utawala wa Aal Khalifa umeendelea kutekeleza sera za ukandamizaji dhidi ya raia wanaopigania mageuzi nchini. Utawala wa Aal Khalifa unaungwa mkono pakubwa na Saudi Arabia, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel; na nchi  hizo zinapinga kuundwa serikali ya wananchi huko Bahrain kwa kuyakandamiza mapambano ya wananchi.  

Ukamdamizaji wa vikosi vya usalama vya Bahrain dhidi ya raia 

Utawala wa ukoo wa Aal Khalifa unatumia njia mbalimbali za ukandamizaji na dhulma dhidi ya wananchi na wanaharakati wa jumuiya za kiraia, na moja ya mbinu hizo ni kuwatia nguvuni na kuwafunga jela. Bahrain katika muongo uliopita imewatia nguvuni karibu watu elfu 15 kwa itikadi zao za kisiasa; na sasa pia wanaharakati wa kisiasa karibu 4500 waliotiwa nguvuni wanaishi katika mazingira magumu kwenye seli na jela za nchi hiyo. Wafungwa wa kisiasa wanateswa na kunyanyaswa na vyombo husika kwa njia na mbinu tofauti. Mingoni mwa mbinu hizo ni kuwashikilia katika seli za mtu mmoja mmoja, kuwanyima huduma za afya zinazofaa, kuwatesa na kuwadhalilisha kingono, kuwalazimisha kukiri makosa ambayo hawakufanya, kuwatesa kwa  nyaya za umeme, kuwafutia haki yao ya uraia, kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela, na pia kuwanyima au kuwapunguzia mawasiliano na familia zao. Mbali na ukandamizaji na dhulma zote hizo dhidi ya wafungwa wa kisiasa huko Bahrain, nchi hiyo mwaka 2017 ilianza tena kutekeleza hukumu ya kunyonga na hadi sasa wafungwa kadhaa wa kisiasa wamenyongwa nchini humo.  

Wafungwa wa kisiasa wa Bahrain 

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita zimetolewa ripoti nyingi kuhusu hali mbaya na ya kutisha ya wafungwa katika jela za utawala wa Aal Khalifa huko Bahrain. Ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu zinaeleza kuwa, raia 26 wa Bahrain wangali wanasubiri hukumu ya kunyongwa. Watu 8 kati ya watuhumiwa hao 26 wametajwa kuwa na hatia na wamehukumiwa kwa mujibu wa hukumu zisizo za kiadilifu baada ya  kulazimika kukiri makosa kwa kulazimishwa kupitia njia ya kuteswa na kudhalilisha pakubwa kingono. Yusuf al Jamri mwanaharakati wa Bahrain ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Wafungwa wa kisiasa wa Bahrain wameeleza kuwa utawala wa Aal Khalifa umewazuia kuwasiliana na familia zao." Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wefaq  ya Bahrain pia hivi karibuni ilitoa taarifa ikieleza kuwa, hadi kufikia sasa wafungwa kadhaa wa kisiasa wameaga dunia katika magereza ya utawala wa Aal Khalifa kutokana na hali mbaya ndani ya jela, kukosekana matibabu, kuteswa na kudhalilishwa kingono ikiwea ni pamoja na kubakwa, n.k. 

Makundi ya kutetea haki za binadamu yameulaani na kuukosoa mara kadhaa utawala wa Aal Khalifa kwa kuwakandamiza wapinzani na yametoa wito wa kufanyika marekebisho katika muundo wa kisiasa nchini humo. Utawala wa Bahrain kwa upande wake unadai kuwa, unawahukumu wapinzani kwa mujibu wa sheria za kimataifa na eti ndio maana hauafiki ukosoaji wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine kuhusu hukumu na sababu za kutiwa nguvuni wapinzani. Familia za wafungwa wa kisiasa na kiitikadi waliohukumiwa kunyongwa zilimuomba Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, kufanya mazungumzo na utawala wa Aal Khalifa kuhusu suala la wafungwa hao sambamba na kutetea haki zao. Familia hizo ziliwasilisha ombi hilo katika ziara ya Papa Francis nchini Bahrain mwezi Novemba mwaka jana. Familia za wafungwa wa kisiasa na kiitikadi huko Bahrain aidha zilimuomba Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani kutonyamazia kimya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na haki za wafungwa wapinzani ambao ni watetezi wa demokrasia unaofanywa na  utawala wa Manama. Hata hivyo baada ya ziara hiyo, utawala wa Aal Khalifa umekithirisha vitendo na ukandamizaji dhidi ya wafungwa wa kisiasa nchini humo. Utawala wa Aal Khalifa unazidisha vitendo vya ukatili ili kuzuia maandamano ya waanchi katika kukaribia maadhimisho ya mwaka wa 12 wa mapambano ya watu wa Bahrain. 

Papa Francis, ziarani nchini Bahrain 

 

Tags