Jan 30, 2023 03:10 UTC
  • Jihadul-Islami: Wapalestina hawakhofu walowezi wa Kizayuni kuzatitiwa kwa silaha

Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema kuwa, Wapalestina hawaogopi wala hawaingiwi na hofu yoyote kwa sababu ya walowezi wa Kizayuni kuzatitiwa kwa silaha.

Chaneli ya 14 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imekiri kuwa, kuanzia Jumamosi hadi sasa makundi ya muqawama ya Palestina yamefanya operesheni 57 dhidi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la Falastin Al-Youm, Muhammad al-Hindi, mjumbe wa ofisi ya kisiasa na mkuu wa kitengo cha siasa cha harakati ya Jihadul-Islamu amesema, taifa la Palestina halitasalimu amri kwa hujuma na uchokozi wa utawala wa Kizayuni na lina azma thabiti ya kukabiliana nao katika miji yote ya Palestina.
 
Al-Hindi amesema, anatazamia Israel itachukua hatua kutokana na operesheni ya kishujaa ya Quds na akaongeza kuwa, taifa la Palestina liko tayari kwa lolote linalowezekana kutokea.

Mjumbe huyo wa Jihadul-Islami amesisitiza kuwa, uamuzi wa Wazayuni wa kuwapa silaha walowezi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas hauwatii hofu wala woga Wapalestina, na maamuzi ya hivi karibuni ya Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa baraza la mawaziri lenye misimamo ya kufurutu mpaka la utawala huo ghasibu yanachukuliwa kwa lengo la kuwapoza na kuwatuliza wazayuni.

 
Al-Hindi ameongeza kuwa, taifa la Palestina halitasalimu amri kwa hujuma na uvamizi wa Israel, na kwamba operesheni ya Ijumaa usiku huko Quds iliyopelekea kuangamizwa Wazayuni wasiopungua wanane, ilikuwa jibu kwa uchokozi na jinai za mtawalia za Wazayuni.
 
Al-Hindi amesema, utawala ghasibu wa Kizayuni unatumia kila nyenzo ya ukatili na utumiaji mabavu kulipgisha magoti taifa la Palestina, lakini Wapalestina hawatasalimu amri katu. Ameongeza kuwa, taifa la Palestina halitasalimu amri kwa adui Mzayuni na liko tayari kukabiliana naye wakati wowote na mahali popote.
 
Jumamosi usiku, wakazi wa Ukanda wa Gaza walionyesha furaha yao kwa operesheni ya kishujaa iliyotekelezwa Quds kwa kugawa vitafunio vitamu na kupiga nara za Takbir huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina.../