May 31, 2023 06:47 UTC
  • Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina yaonya upanuzi wa vitongoji vya walowezi Nablos

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya mamlaka ya ndani ya Palestina imeonya kuhusiana na upanuzi wa vitongojii vya walowezi wa Kizayuni huko Nablos, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imeonya kuhusiana na matokeo mabaya na hatari ya hatua ya walowezi wa Kizayuni wenye silaha ya kuweka mahema katika kitongoji cha Dirastia.

Hatua hiyo inakwenda sambamba na uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Benjamin Netanyahu wa kupasisha mpango mwingine wa upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Hii ni katika hali ambayo, azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakikosolewa kutokana na himaya na uungaji mkono wake kwa utawala ghasibu wa Israel na hata wengi wanaamini kuwa, himaya hiyo ndiyo inayoupa kiburi utawala huo ghasibu.

Tags