Jun 02, 2023 01:45 UTC
  • Luteka ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni, kuendelea kutumia turufu iliyofeli kutatua mgogoro wa ndani

Baraza la Mawaziri la waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu linaendelea kutumia turufu iliyofeli ya kijeshi kujaribu kutatua mgogoro wa ndani unaoikabili serikali ya genge lenye misimamo mikali ya kufurutu mipaka la Kizayuni.

Baraza jipya la mawaziri la Benjamin Netanyahu liliingia madarakani mwezi Januari 2023. Tukio muhimu lililotokea tangu kuundwa serikali hiyo mpya ya Israel, ni maandamano makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia yote ya utawala wa Kizayuni. Watu laki sita hadi laki saba wamekuwa wakishiriki kwenye maandamano ya kila wiki ya wapinzani wa serikali hiyo.

Netanyahu ameemewa na hajui la kufanya mbele ya mgogoro huo mkubwa wa ndani ya Israel ambao unatishia vikali kuporomoka serikali yake. Netanyahu alianzisha vita dhidi ya wananchi wa Ghaza ambacho ni kiungo chenye nguvu kidogo ikilinganishwa na viungo vingine vya kambi ya muqawama, ili ajaribu angalau kupunguza makali ya mgogoro wa ndani ya Israel. Lakini vita hivyo vya siku 5 dhidi ya Ghaza vilizidi kuufedhehesha utawala wa Kizayuni. Katika kipindi hicho cha siku tano, wanamapambano wa Palestina walivurumisha karibu makombora 1,500 na kupiga maeneo ya walowezi wa Kizayuni. Mfumo wa Israel wa kujilinda na mashambulizi ya makombora ulishindwa kabisa kukabiliana na makombora ya wanamuqawama wa Palestina kiasi kwamba gazeti la Kizayuni la Haaretz lilikiri kwamba matokeo mabaya ya vita vya siku tano vilivyoanzishwa na Netanyahu dhidi ya ukanda wa Ghaza si kitu kingine isipokuwa kuzidisha mivutano na mizozo ndani ya jamii ya Wazayuni na kuzidi kuleta mshikamano katika safu za Wapalestina na matokeo ya yote hayo mawili ni kuangamia utawala wa Kizayuni.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

 

Baada ya Netanyahu kushindwa kupata alichotarajia katika vita vya Ghaza na kutokana na kuendelea maandamano ya kila wiki dhidi ya serikalli yake, sasa ameamua kufanya mazoezi ya kijeshi ili kujaribu tena angalau kupuguza makali ya upinzani dhidi yake. Serikali ya Israel imeanzisha mazoezi ya kijeshi ikijifanya kama vile inapigana vita vya pande zote za kutokea upande wa Lebanon, Syria, Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni amesema, luteka hiyo ya kijeshi itafanyika kwa muda wa wiki mbili na itashirikisha vikosi na majeshi yote ya Israel, ya angani, majini na ardhini.

Nukta muhimu kuhusu mazoezi hayo ya kijeshi ya Israel ni malengo yake. Luteka hiyo ya Israel imefanyika siku chache tu baada ya mazoezi ya kihistoria ya kijeshi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon tena kwenye mipaka ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Hivyo luteka hii ya kijeshi ya Israel ni kujaribu kujibu mazoezi ya hivi karibuni ya kijeshi ya Hizbullah ya Lebanon. Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni ilisema kuhusu luteka ya Hizbullah ya Lebanon kwamba, mazoezi hayo ya kijeshi ya harakati hiyo ya Kiislamu ilikuwa na kuitunishia misuli Israel baada ya miaka 23 ya kukimbia wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kusini mwa Lebanon. Ilisema: Hivi sasa Hizbullah ya Lebanon inaujua vyema mgogoro unaoumeng’enya ndani kwa ndani utawala wa Kizayuni na inaelewa kuwa inaweza kutumia vizuri udhaifu wa Israel hivi sasa.

Askari wa Israel wakikandamiza maandamano ya kumpinga Netanyahu mjini Tel Aviv

 

Tunapozingatia hayo yote tutaona kuwa, kama ilivyoripoti kanali ya 12 ya televisheni ya Israel, utawala huo pandikizi hivi sasa umekwama kwenye kinamasi ya mgogoro wa ndani. Vita vya Ghaza vimeshindwa kupunguza makali ya mgogoro huo. Hivyo, lengo jingine la kufanyika mazoezi ya hivi sasa ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni, ni kujaribu kuendelea kutumia turufu iliyofeli ya kijeshi katika kumaliza mgogoro wa ndani ya utawala wa Kizayuni. Lakini hakuna ishara zozote zinazoonesha kuwa mazoezi hayo ya kijeshi yataweza kumaliza mgogoro huo na sababu yake ni kuwa mgogoro wa hivi sasa ndani ya Israel unatokana na kurundikana matatizo chungu nzima na misimamo mikali ya serikali ya Benjamin Netanyahu. Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, mizizi hiyo iliyojikita ndani ya mgogoro huo, haiwezi kung’olewa kwa hila za kuzusha vita na kufanya mazoezi ya kijeshi.