Jun 13, 2024 13:39 UTC
  • Hizbullah yayatwanga kwa maroketi na droni 150 maeneo ya Wazayuni na kuyateketeza kwa moto

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza leo Alkhamisi kwamba, mashambulizi makubwa mapya ya Hizbullah ya Lebanon yaliyotumia makumi ya droni na maroketi yamesababisha moto mkubwa katika maeneo 15 ya milima ya Golan na ya kaskazin mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, vyombo hivyo vya habari vya Israel vimesema kuwa, katika kipindi cha saa moja iliyopita hadi vinatangaza habari hiyo, Hizbullah ya Lebanon ilikuwa imeshashambulia maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu pamoja na milima ya Golan, kwa kutumia kwa uchache droni 30 na maroketi 100 na kusababisha moto mkubwa.

Ving'ora vya tahadhari vimesikika vikilia mfululizo katika maeneo hayo na hadi wakati vyombo hivyo vya habari vya Israel vilipokuwa vinaripoti habari hii, ving'ora hivyo vilikuwa bado vinalia.

Mwanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

 

Baada ya hapo vyombo hivyo vya Kizayuni vimetangaza kuwa, kambi zote za kijeshi za Israel katika maeneo ya Safed na Milima ya Golan zimeshambuliwa leo na kwamba kwa uchache Hizbullah imetumia makombora, maroketi na droni zaidi ya 150 kupiga kambi hizo za Wazayuni. 

Jana Jumatano pia, Hizbullah ya Lebanon ilifanya mashambulizi makali kwa kutumia zaidi ya maroketi 200  kupiga maeneo ya Wazayuni ikiwa ni kujibu jinai za Israel za kuwaua kigaidi wanamapambano wanne wa harakati hiyo ya Kiislamu. Vyombo vya habari vya Israel sambamba na kukiri hasara kubwa zilizosababishwa na mashambulizi hayo ya Hizbullah vimetangaza kuwa, timu 21 za kuzima moto za Israel zilikuwa zinaendelea kuzima moto huo ingawa zilikuwa hazijafanikiwa.

Tags