Jun 18, 2024 08:16 UTC
  • Ndege za kivita za Marekani na Uingereza zashambulia tena magharibi mwa Yemen

Ndege za kivita za Marekani na Uingereza kwa mara nyingine tena zimeshambulia kwa mabomu maeneo ya magharibi mwa Yemen.

Ndege za kivita za Marekani na Uingereza zimeshambulia mara tano mkoa wa Hodeidah ulioko magharibi mwa Yemen. Kufikia sasa, hakuna ripoti zozote zilizotolewa kuhusu uwezekano wa maafa na majeruhi katika mashambulio hayo. Siku chache zilizopita ndege za kivita za Marekani na Uingereza zimeyashambulia maeneo ya kadhaa ya Yemen hasa ya mkoa wa Hodeidah. Nchi mbili hizo za Magharibi pia zimekuwa zikifanya mashambulizi makali katika maeneo mengine ya Yemen katika miezi kadhaa iliyopita.

Mashambulizi hayo yanatekelezwa kwa shabaha ya kutoa mashinikizo dhidi ya serikali ya kitaifa ya Yemen ili iondoe mzingiro wa majini dhidi ya utawala haramu wa Israel. Katika miezi kadhaa iliyopita, jeshi la Yemen limelenga meli kadhaa za Kizayuni au zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) zikiwa katika Bahari Nyekundu hasa katika lango la Bab al-Mandab ili kuunga mkono muqawama wa taifa la Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuendelea kuzishambulia meli za utawala huo au zile zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika Bahari Nyekundu hadi pale utawala wa Kizayuni utakaposimamisha mauaji ya umati na mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Gaza.

Tangu tarehe 7 Oktoba iliyopita, jeshi la Kizayuni limekuwa likiendesha operesheni za mauaji ya kimbari na jinai nyingine za kutisha katika maeneo mbalimbali ya Palestina hususan Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, tangu kuanza kwa mashambulizi hayo ya kinyama kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, jeshi katili la Israel limeua shahidi Wapalestina 37,347 na kujeruhi wengine elfu 85 na 372 katika ukanda huo wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Tags