Jun 20, 2024 08:23 UTC
  • Wasiwasi unaozidi kuongezeka wa Biden kuhusu chokochoko za Netanyahu kusini mwa Lebanon

Amos Hochstein, mjumbe wa Biden, amelitembelea tena eneo la Asia Magharibi ikiwa ni katika juhudi zake za kutuliza hali ya mambo katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Kabla ya hapo, Hochstein aliwasili Tel Aviv na Beirut mnamo tarehe 27 Aprili kwa lengo la kupunguza mvutano kwenye mpaka wa Lebanon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa tovuti ya Kiibrania ya Wala, Hochstein imefanya safari katika eneo kufuatia kuongezeka mvutano katika mpaka wa kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na Lebanon katika siku za hivi karibuni na kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa pande zote mbili ili kuzuia kutokea vita vya pande zote kati ya Hizbullah na Israel.

Amos Hochstein amekutana na Benjamin Netanyahu na Israel Yoav Galant, Waziri Mkuu na Waziri wa Vita wa Israel kwa utaratibu huo ili kuwashawishi wasiishambulie Lebanon, kwa kutilia maanani hatari ya hatua kama hiyo kwa usalama wa Israel.

Ijumaa iliyopita, Jeanine Hennis-Plasschaert, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, na Jenerali Aroldo Lazaro, Mkuu wa kikosi cha UNIFIL nchini humo walitahadharisha juu ya hatari ya kutokea mzozo mkubwa katika eneo hilo katika taarifa yao ya pamoja, wakisisitiza kwamba wana wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano wa hivi sasa na kuziomba pande zote katika eneo la "mstari wa bluu" kuweka kando silaha zao na kutumia njia za amani kutatua matatizo yaliyopo.

Awali, kanali ya CBS iliripoti kwamba kuongezeka mivutano kati ya Israel na Hizbullah ya Lebanon kumewatia wasiwasi viongozi wa serikali ya Washington ambapo wanahofia kuwa huenda Marekani ikasukumwa kwenye vita vikubwa zaidi katika eneo hilo.

Picha zilizochukuliwa karibuni na droni za Hizbullah, za maeneo nyeti ya kiusalama na kiuchumi ya Israel

Mwanzoni mwa vita vya Gaza, mapigano hayo ya hapa na pale yalibanwa kwenye eneo la takriban kilomita 4 tu (maili 2.5) katika pande mbili za mpaka wa Lebanon na ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel; lakini sasa mashambulizi yanatekelezwa ndani zaidi ambapo Hizbullah inashambulia maeneo yaliyo umbali wa kilomita 35 ndani ya Palestina, nayo Israel inalenga maeneo yaliyo umbali wa zaidi ya kilomita 120 ndani ya Lebanon.

Ni wazi kuwa vita kati ya Israel na harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon vitazidisha pakubwa mgogoro wa kieneo na kuihusisha zaidi Marekani katika mgogoro huo. Huo ndio ukweli  wa mambo ambao umewafanya viongozi wa White House wafanye juhudi zaidi za kuzuia mgogoro kama huo usitokee.

Utawala wa Biden una wasiwasi kwamba Tel Aviv itaingia au kuingizwa kwenye vita na Hizbullah bila ya kuwa na mkakati madhubuti wa kupigana vita au kuzingatia athari hasi za vita hivyo.

Vita vya kusini mwa Lebanon, kama vilivyo vya Gaza na vile vile vita vinavyoendelea huko Ukraine, vyote kwa pamoja au kwa namna tofauti vimewatia wasi wasi mkubwa viongozi wa Marekani, na ndio maana wakaamua kumtuma Hochstein huko Tel Aviv na Beirut kwa ajili ya kupunguza mivutano kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Mwezi Oktoba 2022, Lebanon na utawala ghasibu wa Israel zilitia saini makubaliano ya kuainisha mipaka ya baharini kwa upatanishi wa Hochstein, mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani, jambo ambalo lilitajwa na Hizbullah kuwa ushindi mkubwa kwa serikali, watu na muqawama wa Lebanon.

Wakati huo huo, mjumbe huyo wa Marekani anatarajia kukamilisha kwa mafanikio kile ambacho Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje hakuweza kukifanya katika safari zake zote 8 katika eneo hilo katika siku za karibuni.

Hata kama Netanyahu anahitaji kushadidisha vita vya Lebanon kwa ajili ya kulinda mabaki ya serikali yake dhaifu na yenye misimamo mikali, na wakati huo huo kuhamishia kwingine migogoro yake ya ndani, lakini duru nyingi za Kizayuni zinahofia madhara ya kuingia katika vita vya nchi kavu na Hizbullah na zina wasiwasi mkubwa kuhusu matokeo yake.

Ishaq Brik, jenerali mstaafu wa jeshi la Israel amesema shambulio lolote la kijeshi dhidi ya Lebanon ni "wendawazimu" na kuwa uamuzi wowote wa Netanyahu kuishambulia Hizbullah utasababisha maafa makubwa kwa Israeli na hili linatokana na ukweli kuwa utawala huo ghasibu hauna uwezo wa kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani za Hizbullah.

Maeneo ya Wazayuni yaliyoteketezwa karibuni na Hizbullah

Shaul Amsterdamski, mchambuzi wa masuala ya uchumi katika mtandao wa Kan, anasema: "Waisraeli wanapaswa kutambua kwamba vita kamili na Hizbullah huko kaskazini vitakuwa na madhara makubwa sio tu kwa sekta ya kijeshi, bali pia kwa sekta ya uchumi ambapo umeme bila shaka utaathiriwa na vita hivi. Hivyo juhudi zote zinapaswa kufanywa ili kuizuia Israeli isianzishe vita dhidi ya Hizbollah."

Kwa mujibu wa wachunguzi wa mambo, iwapo muqawama wa Lebanon utalazimishwa kuingia kwenye vita, huo utakuwa ni upumbavu mkubwa na hatari zaidi ambao Israel itakuwa imeufanya. Hii ni kwa sababu Hizbullah tayari imechosha na kumkatisha tamaa adui Mzayuni. Imeteketeza moto vitongoji vya utawala huo katika eneo la kaskazini, imeharibu kambi zake za kijeshi na kuwafanya walowezi laki mbili wa Kizayuni walikimbie eneo hilo la kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na walowezi wa Kizayuni. Kwa upande mwingine, kupamba moto vita kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kutamaanisha kujiunga pande zote za muqawama katika vita hivyo kwa manufaa ya muqawama wa Lebanon, hivyo Hizbullah haitaachwa peke yake katika vita hivyo.