Jun 23, 2024 02:44 UTC
  • Sababu na matokeo ya kufunguliwa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Iraq

Ofisi ya masuala ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas hivi karibuni imefunguliwa kwa njia isiyo rasmi huko Baghdad na imepangwa kufunguliwa rasmi katika siku chache zijazo.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas ndiye mhusika muhimu zaidi wa mrengo wa muqawama katika vita vya hivi sasa vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Vikosi vya Qassam, ambalo ni tawi la kijeshi la Hamas na Ofisi ya Kisiasa ya Hamas yanaweza kuchukuliwa kuwa matawi mawili makuu ya harakati hiyo ya muqawama.

Makao makuu ya ofisi ya kisiasa ya Hamas yako mjini Doha, Qatar, lakini katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na tetesi za kuhamishiwa ofisi  hiyo nje ya Doha, tetesi ambazo zimekuwa zikikanushwa mara kwa mara na pande zote za Qatar na Palestina.

Hii ni katika hali ambayo Hamas inapanga kuhuisha shughuli zake nchini Syria na kufungua ofisi yake nyingine nchini Yemen. Kufunguliwa ofisi ya kisiasa ya Hamas huko Iraq kuna ujumbe na sababu kadhaa muhimu.

Sababu kuu ya hatua hiyo ya Hamas ni kufikisha ujumbe huu kwa maadui na wapinzani wake kwamba sio tu kuwa Hamas haijaangamizwa na vita vya miezi 9 vya utawala wa Kizayuni na uungaji mkono wa pande zote wa nchi za Magharibi kwa utawala huo katili, bali shughuli zake zimeimarika hadi nje ya mipaka ya Qatar ambapo ina uwezo wa kuboresha uwezo wake na pande nyingine muhimu za kieneo. Hivyo haionekani kwamba kufunguliwa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Iraq kunamaanisha mwisho wa shughuli zake huko Qatar.

Ufunguzi wa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Iraq una ujumbe muhimu.

Kufunguliwa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Iraq 

Ujumbe na nukta muhimu ni kwamba, mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza yameimarisha umoja na mshikamano wa makundi ya muqawama kuhusu vita vya Gaza. Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, Harakati ya Muqawama wa Kiiislamu ya Ansarullah ya Yemen na Hashd al-Shaabi ya Iraq zinatoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Wapalestina dhidi ya Wazayuni. Kufunguliwa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Iraq pia kunaimarisha mfungamano na umoja wa mhimili wa mapambano katika eneo, na hii ni moja ya matokeo muhimu ya vita vya Ukanda wa Gaza.

Jambo jingine muhimu kuhusu kuwepo Hamas nchini Iraq ni kwamba sasa nafasi ya muqawama wa Iraq katika mhimili wa muqawama itaimarika zaidi.

Kuhusu vita vya Gaza, makundi ya muqawama wa Iraq yamekuwa yakishambulia vituo vya kijeshi vya Marekani kama ishara ya kupinga uungaji mkono wa pande zote wa nchi hiyo kwa jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na wakati huo huo kusaidia muqawama wa Palestina kwa kushambulia vituo muhimu vya utawala huo huko Ashdod na bandaria ya Haifa.

Ujumbe mwingine muhimu ni kwamba, serikali ya Iraq ambayo inaiunga mkono Palestina tangu mwanzoni mwa mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, kwa upande mmoja imeimarisha shughuli za muqawama katika ardhi ya nchi hiyo na kwa upande mwingine kuongeza kiasi kikubwa misaada yake ya kibinadamu inayotumwa huko Ukanda wa Gaza, hadi kufikia kiwango cha nchi inayotuma misaada mingi zaidi Palestina.

Kupitia mahusiano waliyoanzisha na serikali ya Iraq, viongozi wa Hamas wamekuwa wakiwafahamisha wenzao wa Iraq kuhusu undani na matokeo ya mazungumzo kuhusu kadhia ya Palestina, jambo ambalo limepelekea kuimarika uhusiano kati ya Iraq na harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina.

Hivyo Iraq sasa ina nafasi sawa na ya Qatar na Misri kuhusu mgogoro wa Palestina.

Kutokana na uwepo wa makundi mengi ya muqawama nchini Iraq, tunaweza kutarajiwa kwamba katika siku zijazo nchi hii itakuwa na nafasi muhimu zaidi katika mgogoro wa Palestina hata kuliko Misri na Qatar.