Jun 23, 2024 11:13 UTC
  • Harakati za muqawama za Yemen na Iraq zapiga kwa pamoja meli za Wazayuni katika bandari ya Haifa

Msemaji wa Jeshi la Yemen ametangaza leo Jumapili kwamba vikosi vya nchi hiyo kwa kushirikiana na vikosi vya muqawama wa Kiislamu vya Iraq vimelenga meli tano katika bandari ya Haifa na Bahari ya Mediterania katika operesheni ya pamoja.

Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema katika taarifa yake hiyo kwamba: Katika operesheni ya kwanza, meli nne za Wazayuni zimepigwa katika bandari ya Haifa kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zikiwemo meli 2 zilizobeba saruji na meli 2 za mizigo.

Operesheni hiyo imefanywa kwa pamoja na vikosi vya Yemen na harakati za mapambano ya Kiislamu za Iraq. 

Msemaji huyo wa jeshi la Yemen ameongeza kuwa: Katika operesheni ya pili, meli ya Shorthorn Express imelengwa na shambulio la ndege isiyo na rubani katika Bahari ya Mediterania.

Akieleza kuwa operesheni hizo mbili zimeendeshwa kwa mafanikio na kuongeza kwa kusema: "Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutaendelea kuendesha operesheni zetu za kijeshi za pamoja na muqawama wa Kiislamu wa Iraq kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina."

Mwishoni mwa taarifa yake, Jenerali Saree amesisitiza kuwa, operesheni za jeshi la Yemen na makundi ya muqawama wa Kiislamu wa Iraq zitaendelea hadi mwisho wa uchokozi na kuondolewa mzingiro wa wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza.

Katika miezi kadhaa iliyopita, na ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono muqawama wa taifa la Palestina katika Ukanda wa Ghaza, jeshi la Yemen limekuwa likipiga meli na vyombo vya bahari vikiwemo vya Marekani, Uingereza na vya utawala wa Kizayuni vinavyoelekea katika ardhi za Palestina kupitia Bahari Nyekundu na lango Bahari la Bab al-Mandab.