Hamas: Madai ya Israel kuwa imewalenga viongozi wa muqawama Khan Yunis ni ya uongo wa kuficha jinai zake
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas) jana Jumamosi ilikanusha madai ya Israel kwamba jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Al-Mawasi huko Khan Yunisna kuua shahidi wakimbizi 71 wa Kipalestina na kujeruhi wengine karibu 300 zililenga viongozi wa Palestina ni madai ya uongo yenye shabaha ya kuficha jinai za Israel katika eneo hilo.
Katika taarifa yake hiyo, HAMAS imesema kwamba, hii si mara ya kwanza kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kutoa madai kama hayo na kuongeza kuwa, madai hayo ya uongo ya Israel yanalenga kuficha ukubwa wa mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Wazayuni makatili huko Al-Mawasi, Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Taarifa hiyo ya HAMAS imetoa ufafanuzi zaidi kwa kusema: Mauaji dhidi ya wakimbizi wa Palestina wasio na ulinzi wala hatia huko Al-Mawasi, eneo ambalo utawala wa Kizayuni ulidai ni salama kwa ajili ya kukimbilia Wapalestina, ni mauaji ya maangamizi ya kizazi ambayo hayahalalishiki kwa jambo lolote lile na ni mwendelezo wa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina. Katika taarifa yake hiyo kali ya jana Jumamosi, HAMAS imeishutumu na kuilaani pia Marekani kwa kuwa mshirika wa moja kwa moja wa jinai hizo.
Sehemu moja ya taarifa hiyo ya imesema: "Kulenga eneo lenye watu zaidi ya 80,000 waliokimbia makazi yao ni uthibitisho kwamba utawala wa Kizayuni umeamua kwa makusudi kuendelea kufanya jina za maangamizi ya umati dhidi ya watu wetu."
Mapema jana asubuhi, redio ya Jeshi la Israel ilidai kuwa eti shambulio hilo lilimlenga Muhammad Al-Deif, Kamanda wa Brigedi za Al-Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas na Rafi Salama, kamanda wa Brigedi ya Al-Qassam huko Khan Yunis madai ya uongo ambayo yamekanushwa vikali na HAMAS ambayo imesisitiza kuwa, hii si mara ya kwanza kwa utawala wa Kizayuni kueneza propaganda za uongo kama hizo.