Utawala wa Kizayuni waingiwa na hofu na kiwewe cha kukabiliwa na jibu kali la Iran na muqawama
Viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanapitia kipindi kigumu cha hofu, kiwewe na wasiwasi wakisubiri jibu kali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi ya muqawama kutoka na kitendo chao cha kumuua kigaidi Shahidi Ismail Haniyeh, Kiongozi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas alipokuwa safarini mjini Tehran.
Huku akihofia jibu kali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na waitifaki wake wa mhimili wa muqawama katika eneo, Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa kibaguzi wa Israel ametaka kuundwa muungano wa kuulinda utawala huo dhidi ya mashambulio hayo ya kulipiza kisasi.
Wizara ya Vita ya Kizayuni imetangaza kuwa katika mazungumzo yake na John Haley, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Gallant amezungumzia utayari na uwezo wa jeshi la utawala huo katika kuilinda Israel katika nyanja zote lakini wakati huo huo akasisitiza umuhimu wa kuundwa muungano wa kuilinda Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi ya muqawama.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimesema kuwa utawala wa Kizayuni uko katika hali ya tahadhari kubwa kutokana na uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kilipiza kisasi ya makundi ya muqawama kufuatia mauaji ya kigaidi uliyoyafanya dhidi ya shakhsia wawili wakuu wa mhimili wa muqawama. Baada ya mhimili wa muqawama kutishia kutoa jibu kali la kulipiza kisasi cha mauaji ya hivi karibuni dhidi ya Shahidi Ismail Haniyeh na Shahidi Fuad Shukr, hali ya vita vya kisaikolojia imeukumba utawala huo wa Kizayuni.
Shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na utawala katili wa Israel kwenye makazi yao kaskazini mwa Tehran mapema Jumatano iliyopita.
Katika ujumbe wake wa salamu za rambirambi za kuuawa shahidi Ismail Haniyeh, kiongozi shujaa, shupavu, mujahid na mashuhuri wa Hamas kwa Umma wa Kiislamu, mhimili wa muqawama na taifa la Palestina, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa utawala wa Kizayuni kwa kutekeleza jinai na ugaidi huo umejiandalia mazingira ya kuadhibiwa vikali na kusema kuwa ni jukumu la Iran kulipiza kisasi cha damu ya kiongozi huyo iliyomwaga katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Matokeo ya jinai za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza katika miezi ya hivi karibuni, yamedhihirisha utayari kamili wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na makundi ya muqawama, wa kuuadhibu utawala wa kibaguzi wa Israel.
Katika miezi ya hivi karibuni, Hizbullah ya Lebanon na makundi mengine ya muqawama yamekuwa yakikabiliana vikali na utawala wa Kizayuni katika medani ya vita na kutoa mapigo yasiyoweza kufidika kwa Wazayuni. Kuuawa shahidi Ismail Haniyeh kumepelekea kuwepo umoja na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya makundi ya muqawama ili kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani na washirika wengine wa jinai za Tel Aviv katika eneo.
Operesheni za Hizbullah ya Lebanon na makundi mengine ya muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel zinaashiria wazi utayari wa makundi hayo katika kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni. Ni wazi kuwa viongozi wa utawala wa Kizayuni ambao ndio chanzo kikuu cha mivutano na migogoro katika eneo, wanapaswa kuwa na wasi wasi, woga na hofu kuhusu matokeo ya vitendo vyao hivyo viovu.
Mapigano ya kimbinu na utumiaji wa uwezo wa kijeshi ni jambo lenye taathira kubwa katika kuadhibu utawala wa Kizayuni ambao siku zote haujakuwa na lengo jingine isipokuwa kufanya jinai na mauaji ya umati dhidi ya watu madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina.
Katika kujibu mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, kupitia "Operesheni ya Ahadi ya Kweli" Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kuwa ina zana mbalimbali na za hali ya juu za kuwaadhibu wachokozi.
Kupanuka Operesheni za muqawama katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa sababu ya kudhoofika na kukaribia kusambaratika utawala wa Kizayuni, katika hali ambayo mtazamo mzuri na uungaji mkono wa watu wa eneo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na muqawama umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika siku za karibuni.
Mkondo wa matukio katika eneo unaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu vikali vitendo viovu na vya kichokozi vya Wazayuni.