Aug 04, 2024 07:24 UTC
  • Shirika la Redio na TV la Israel: Hatupati usingizi kwa hofu ya majibu ya Iran

Shirika la Redio na Televisheni la utawala wa Kizayuni wa Israel limekiri kwamba Wazayuni hawapati usingizi kabisa kwa kuhofia jibu la Iran hasa kwa kutojua majibu hayo yatatolewa lini na kutabiri kuwa, huenda mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Tehran yatapiga kambi za kijeshi za Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, utawala wa Kizayuni hivi sasa umepoteza kabisa usingizi hasa kwa sababu haujui majibu ya kambi ya muqawama dhidi ya jinai za utawala huo yatafanyika lini, kutokea wapi na kwa kiwango gani.

Kambi ya muqawama ikiongozwa na Iran imetangaza wazi kuwa itatoa majibu makali kwa jinai ya Israel ya kuwaua shahidi makamanda wa Muqawama, Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS na Fuad Shukr, kamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon.

Shirika la Redio na Televisheni la Israel lilikiri jana Jumamosi kwamba katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, kuna hofu kubwa kutokana na majibu ya Iran na ni kama vile maeneo yote ya utawala wa Kizayuni yamefungwa. 

Kwa upande wake gazeti la Marekani la Wall Street Journal liliandika jana kuhusu jibu la Iran kwa mauaji ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran, kwamba, wakati jeshi la Israel lilitangaza siku ya Ijumaa kuwa liko katika hali ya tahadhari kubwa, viongozi wa Marekani wanajaribu kukusanya zana za kijeshi na kuhamasisha washirika wao wa kikanda kukabiliana na majibu hayo ya Iran.