Umoja wa Wapalestina katika Siku ya Kitaifa na Kimataifa ya kuunga mkono Ghaza na mateka wa Kipalestina
Miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan imeshuhudia maandamano ya kupinga vita vya Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na mauaji ya kimbari dhidi yao katika siku ya kitaifa na kimataifa ya kuisaidia na kuiunga mkono Ghaza na mateka Wapalestina.
Katika taarifa hiyo ya Julai 28 aliyoitoa siku tatu kabla ya kuuawa shaahidi, Haniya aliashiria -kuendelea kwa mwezi wa 10 mtawalia jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, kuongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa idadi ya mateka Wapalestina waliouawa shahidi katika jela za Kizayuni, udhibiti wa kiwango cha juu wa taarifa kuhusu hali za mateka hao, kunyongwa majangwani Wapalestina waliotekwa nyara Ghaza na kuwekwa kwenye mahabusu za utawala wa Kizayuni, kimya cha Jamii ya Kimataifa kuhusiana na Vita vya Ghaza na kushindwa kwake kuvisimamisha vita hivyo, upendeleo na ushiriki kamili wa Marekani katika vita vya Ghaza na kushindwa kwa taasisi za kimataifa kutimiza wajibu wao-; na kwa sababu ya yote hayo akaitangaza Agosti 3 kuwa Siku ya Kitaifa na Kimataifa ya kuisaidia Ghaza na mateka Wapalestina.
Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas pamoja na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Jumatano Julai 31 katika shambulio lililolenga jengo la makazi aliyofikia hapa jijini Tehran. Pamoja na hayo, wananchi wa Palestina katika miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan waliitikia mwito wa Shahidi huyo, wakajitokeza mabarabarani katika siku ya kitaifa na kimataifa ya kuiunga mkono Ghaza na mateka Wapalestina na wakalaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni.
Wakati hayo yanajiri, Sheikh Mustafa Abu Arra, mmoja wa viongozi wa harakati ya Hamas, alikufa shahidi siku chache zilizopita kutokana na dharau aliyofanyiwa ya kutopatiwa huduma za afya na suhula za tiba ndani ya jela ya utawala wa Kizayuni. Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ilitoa pole kwa kuuawa shahidi Sheikh Mustafa Abu Arra katika jela ya utawala wa Kizayuni na kuubebesha utawala huo dhima kamili ya mauaji hayo.
Utawala wa Kizayuni umeshadidisha vitendo vyake vya kinyama dhidi ya wakazi wa Ghaza tangu ilipotekelezwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na makundi ya Muqawama ya Palestina na kutokana na kushindwa Wazayuni kukabiliana na muqawama huo; na hausiti kufanya vitendo vyovyote vile vya kikatili dhidi ya Wapalestina. Nayo Marekani na waungaji mkono wengine wa Magharibi wa utawala wa Kizayuni wameamua kunyamaza kimya licha ya kuwa na uelewa kamili wa faili chafu la Wazayuni na jinai zao za kinyama wanazowafanyia Wapalestina.
Kufanya maandamano na kutangaza mshikamano Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutazidisha umoja na maelewano kati ya wananchi wa Palestina; na mchakato huo utayafanya makundi ya Muqawama wa Palestina yawe tayari zaidi kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Kuadhimisha siku ya kitaifa na kimataifa ya kuisaidia na kuiunga mkono Ghaza na mateka Wapalestina kutawafanya walimwengu pia wawe na uelewa sahihi kuhusu hali ya sasa ya Palestina na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza. Kuzima propaganda za vyombo vya habari vya Magharibi na Marekani na kutangazwa habari sahihi na za kweli za vita vya Ghaza kutawafanya walimwengu wazidi kubainikiwa na jinai za utawala wa Kizayuni.
Wakati huohuo, mshikamano na ushirikiano wa Ulimwengu wa Kiislamu ni jambo muhimu zaidi linaloweza kuwa na taathira katika kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni na kuwaunganisha pamoja watetezi wa amani na wapinzani wa mwenendo wa Wazayuni wa kushupalia vita. Katika miezi ya hivi karibuni pia, mshikamano wa nchi za Kiislamu katika kuunga mkono Ghaza na kusimama dhidi ya utawala wa Kizayuni umekuwa na matokeo chanya na athirifu, kiasi kwamba Wazayuni wametengwa zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote.../