Aug 05, 2024 07:26 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon yalenga makao ya kamandi ya utawala katili wa Israel

Hizbullah ya Lebanon imelenga makao ya Kamandi ya Kitengo cha 91 cha utawala wa Kizayuni huko Eilat katika shambulizi jipya dhidi ya Bandari ya Eilat katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, kwa kutumia ndege kadhaa zisizo na rubani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hizbullah ya Lebanon imetangaza katika taarifa  kwamba Mujahidina wa Muqawama wa Kiislamu katika kuunga mkono wananchi wanamapambano wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na kujibu mashambulizi na mauaji ya adui Mzayuni katika miji ya Al-Bazurieh, Deirsarian na Howleh kusini mwa Lebanon, imetumia ndege kadhaa zisizo na rubani kulenga makao mapya ya Kitengo cha 91 cha Israeli katika Bandari ya Eilat.

Vituo vingine vya jeshi la utawala wa Israel vimelengwa na Hizbullah

Taarifa hiyo ya Hizbullah ya Lebanon, imeeleza kuwa maeneo ya maafisa na askari wa Kizayuni yamelengwa moja kwa moja ambapo idadi kubwa ya Wazayuni wameuawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Vyombo vya habari vya utawala ghasibu wa Israel pia vimetangaza kuwa ripoti ya awali inaonyesha kuwa hasara kubwa imepatikana kufuatia "kuanguka" ndege isiyo na rubani katika mji wa Illit Hashaher.

Tovuti ya habari ya Al-Ahad ya Lebanon pia imeripoti kuwa kutokana na shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye eneo la "Illi Hashahr", eneo hilo liliwaka moto na wanajeshi wawili wa Kizayuni wakajeruhiwa vibaya sana.

Tangu utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina uanzishe vita vya mauaji ya halaiki huko Ukanda wa Gaza mapema mwezi Oktoba 7 mwaka jana, Hizbullah ya Lebanon, imekuwa ikifanya operesheni kubwa za jeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa lengo la kuushughulisha utawala huo katika eneo hilo na hivyo kupunguza mashinikizo ya utawala huo dhidi ya muqawama na watu wa Gaza.

Tags