Aug 06, 2024 12:03 UTC
  • Bezalel Smotrich
    Bezalel Smotrich

Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, amesema kwamba vifo vya Wapalestina milioni mbili katika Ukanda wa Gaza kutokana na njaa "vinaweza kuwa vya haki na uadilifu kwa ajili ya kuwarejesha mateka wa Israel," wanaoshikiliwa na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina.

Smotrich ambaye ni miongoni mwa mawaziri wenye misimamo ya kupindukia mipaka katika baraza la mawaziri la Israel, ameongeza kuwa, haiwezekani kuangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kijeshi na kiraia bila ya kudhibiti misaada ya kibinadamu.

Waziri huyo wa Fedha wa Israel pia amekariri upinzani wake dhidi ya suala la kuhitimishwa vita na kubadilishana mateka na wafungwa na makundi ya Wapalestina huko Gaza, akidai kuwa: "Nadhani hawapaswi kuachiliwa huru kwa sababu watarudi kuwaua Wayahudi."

Israel inashikilia Wapalestina wasiopungua 9,500 katika magereza yake, na inakadiria kuwepo kwa mateka 115 wa Israel huko Gaza. Harakati ya Hamas imetangaza kuwa mateka zaidi ya 70 wa Israel wameuawa katika mashambulizi ya kiholela ya jeshi la Israel.