Aug 09, 2024 02:46 UTC
  • Madhara na uharibifu wa kinyama unaofanywa na Wazayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel haujajiwekea mipaka yoyote katika mauaji ya halaiki na ya kimbari unayofanya dhidi ya wananchi wa Palestina. Askari wenyewe wa jeshi la utawala huo dhalimu wamekuwa wakikiri waziwazi na bila ya hofu kwamba wanawaua makusudi Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza.

Katika mahojiano na televisheni ya CNN, baadhi ya askari walioamua kuacha kazi katika jeshi la utawala bandia wa Israel wameeleza kuwa, wamechoshwa na mbinu za kivita za kinyama zinazotumiwa na jeshi hilo huko Ghaza na kwamba hawakuweza kuustahamili uharibifu mkubwa uliofanywa wa kiwango walichoshuhudia katika eneo hilo.
 
CNN imetayarisha ripoti kuhusiana na suala hilo inayoonyesha upeo wa juu kabisa wa ukatili na jinai zilizofanywa na Wazayuni. Askari wachache wa jeshi la Israel ambao hawakuweza kuvumilia kiwango hicho cha ukatili walioshuhudia wameamua kuacha kazi katika jeshi hilo la Kizayuni. Ripota wa CNN amezungumza na baadhi ya wanajeshi hao ambao wameamua kusimulia sehemu ndogo tu ya jinai za Wazayuni katika mauaji ya kimbari wanayofanya dhidi ya Wapalestina.
Michael Ofer Ziv

Michael Ofer Ziv, ni mmoja wa askari walioacha kazi katika jeshi la Israel, akiwa kamanda anayesimamia mashambulizi ya anga na kuwasimamia pia askari wa utawala huo wa Kizayuni walioko Ghaza. Ofer Ziv, ambaye alishuhudia uharibifu uliofanywa wa majengo ya Ghaza anasema, ili kuweza kulifanya hilo kwa urahisi zaidi, mwanzoni alijaribu kutasawiri kwamba, hakuna uhusiano wowote kati ya ukweli halisi na taswira za kidijitali alizoona mbele ya macho yake, kwa kuchukulia kwamba, ni kama alikuwa akicheza michezo ya kompyuta tu. Askari huyo wa jeshi la utawala bandia wa Israel anasema, lakini baada ya muda, hakuweza tena kuukana ukweli kwamba, makumi ya raia wa Palestina walikuwa wakifariki ndani ya majengo yaliyokuwa yakibomolewa na kuteketezwa mbele ya macho yake.

Yuval Green, mwanajeshi mwingine ambaye kwa muda fulani alihudumu kama daktari wakati wa mashambulio ya jeshi la Kizayuni huko Ghaza yeye anasema, katika siku za mwanzo baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, hamu ya kulipiza kisasi dhidi ya Hamas ilimchochea sana kushiriki katika vita, lakini baadaye kidogo, akang'amua malengo halisi ya kijeshi ya Wazayuni katika vita hivyo.
Green, ambaye alipigwa na butwaa kutokana na mawazo na mitazamo ya kinyama waliyokuwa nayo makamanda wake anasema: "fikra kama za kuwaua watu wote wa Ghaza zilionekana ghafla kuwa jambo la kawaida kabisa!"
Yuval Green

Ukweli ni kuwa, jinai wanazofanya askari wa jeshi la Israel huko Ghaza zinatokana na fikra za ubaguzi wa rangi walizonazo viongozi wa utawala huo wa Kizayuni. Kabla ya hapo, viongozi wa utawala huo haramu walikuwa wameshatamka kuwa hawawaoni Wapalestina kuwa ni binadamu na kwamba inajuzu kuwaua kwa kutumia mbinu yoyote ile.

 
Itakumbukwa kuwa saa chache kabla ya kushambuliwa Hospitali ya Al-Ma'adani huko Ghaza, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu mbaguzi wa rangi wa utawala bandia wa Israel, aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba: "haya ni makabiliano kati ya watoto wa nuru na watoto wa giza; kati ya utu na sheria ya msituni."
Israel ni utawala wa kibaguzi wa Apathaidi; lakini huko Gaza umekwenda mbali zaidi ya hapo na kufika hadi ya kukana hata kizazi za wanadamu. Haya ni matamshi aliyotamka kinagaubaga waziri wa vita wa Israel Yoav Gallant aliposema: "sisi tunapigana na wanyama wenye dhahiri ya kibinadamu!" Bila shaka, kauli hii si msimamo wa kihisia tu uliotangazwa katika hali hasasi, bali ni imani inayokubalika mbele ya Wazayuni.

Naye Naftali Bennett, waziri wa elimu na waziri mkuu wa zamani wa Israel amesema: "ni wazi kwamba sisi tunamnyima adui yetu maji na umeme." Gideon Levy, mwandishi wa gazeti la Haaretz, anasema: "kuwavua utu Wapalestina kunakofanywa kwa uratibu maalumu" ni moja ya sababu kuu za ukimya unaoonyeshwa mbele ya hali halisi ya kutisha inayoshuhudiwa.

Mwenendo wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina na kuwavua utu wao wakazi hao halisi wa ardhi ya Palestina si jambo geni. Kwa miaka 75 sasa, Israel imekuwa ikiangamiza kizazi na ardhi ya Wapalestina kwa kutekeleza nadharia potofu na ya uzushi ya "ardhi isiyo na watu kwa ajili ya watu wasio na ardhi" kwa uungaji mkono kamili wa madola ya Magharibi.  
Wazayuni, ambao wanajiona kuwa ni "kaumu teule" na ambayo eti imedhulumika, wanajipa haki ya kufanya lolote lile watakalo, ikiwa ni pamoja na kuvamia na kukalia ardhi kwa mabavu, kuwafukuza na kuwaua wenyeji wa ardhi wanazozivamia, na wakati huo huo kuwavua utu wao watu hao.

Hata hivyo, licha ya njama na jinai zote wanazofanya Wazayuni, hivi sasa vuguvugu la Muqawama katika kizazi cha pili na cha tatu cha Wapalestina waliolazimishwa kuhama makazi yao, lina nguvu zaidi kuliko la vizazi vilivyotangulia vya Palestina. Kizazi hiki kimezaliwa na kukulia kwenye mazingira ya ghadhabu na chuki dhidi ya Wazayuni. Wapalestina wa kizazi hiki hawataachana na piganio lao tukufu, bali wataendeleza piganio hilo la kuikomboa Palestina maadamu utawala bandia na haramu wa Israel unaendelea kuwepo. Mauaji ya halaiki ya Wapalestina yataifanya irada na hamasa ya Muqawama wa kupambana na Wazayuni iwe kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma../