Palestina yaitaka ICC kumkamata Smotrich baada ya kutoa wito wa kuuawa Wapalestina mil. 2 kwa njaa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa hati ya kukamatwa Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, kwa sababu ya wito wake wa kuwaua kwa njaa Wapalestina milioni mbili huko Gaza.
Ombi hili la serikali ya Palestina limetolewa baada ya vita vya Israel, vinavyoungwa mkono na Marekani, vinavyoendelea kwa zaidi ya miezi 10, kuua na kujeruhi zaidi ya Wapalestina 131,000, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, na wengine zaidi ya 10,000 wametoweka.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeyataja matamshi ya Bezalel Smotrich kuwa ni kielelezo cha sera za mauaji ya kimbari na kueleza kuwa matamshi hayo hayakulaaniwa na serikali ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Pia imesisitiza kwamba alichosema Smotrich ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Kufuatia hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuchukua hatua za haraka dhidi ya Smotrich na kuitaka jamii ya kimataifa kulaani msimamo huo na kumuwekea vikwazo waziri huyo wa Israel.
Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, amesema kwamba kuwaua Wapalestina milioni mbili katika Ukanda wa Gaza kwa na njaa "kunaweza kuwa haki na uadilifu kwa ajili ya kuwarejesha mateka wa Israel," wanaoshikiliwa na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina.
Kauli hiyo ya ya Smotrich imeshutumiwa vikali kimataifa, huku Umoja wa Ulaya ukiilaani na kusema kuwa ni uhalifu wa kivita.