Aug 10, 2024 07:30 UTC
  • Israel yaua Wapalestina zaidi ya mia moja na kujeruhiwa makumi kwenye eneo la ibada huko Gaza

Zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mauaji mapya yaliyofanywa na utawala vamizi wa Israel katikati mwa mji wa Gaza alfajiri ya leo, Jumamosi.

Ripoti zinasema kwamba utawala huo vamizi umeshambulia kwa bomu shule ya "Al-Tabieen" katika kitongoji cha Al-Daraj baada ya Swala ya Alfajiri na kwamba idadi ya waliouawa inaweza kuongezeka kutokana na kuwepo kati ya watu 4,000 hadi 5,000 katika shule hiyo iliyopo kwenye mtaa wa Al-Nafaq.

Ripoti zinasema kuwa shambulio hilo limelenga moja kwa moja eneo la ibada la shule hiyo kwa makombora matatu wakati Wapalestina waliokimbia makazi yao walipokuwa wakifanya ibada ya Swala ya Alfajiri, na kwamba miili ya wahanga hao ilirundikana, maiti zikiwa juu ya nyingine.

Ripoti za walioshuhudia zinasema, timu za madaktari zimelazimika kukusanya mabaki ya baadhi ya mashahidi pamoja katika sanda moja, kutokana na kushindwa kutambua wenye miili hiyo.

Idara ya Ulinzi wa Raia katika eneo la Gaza imesema kuwa miili ya raia imeteketea kwa moto kutokana na shambulio la Israel katika shule hiyo, ikibainisha kuwa wafanyakazi wa idara hiyo wanajaribu kudhibiti moto huo ili kuopoa miili ya mashahidi na kuokoa majeruhi.

Tags