Ripota wa UN: Israel inafanya mauaji ya kimbari Gaza kwa silaha za US, Ulaya
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu amekosoa vikali hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuendelea kufanya mauaji na jinai nyingine za kutisha dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Francesca Albanese amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia silaha za Marekani na nchi za Ulaya kuendeleza mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Albanese alisema hayo jana, katika radiamali yake kwa mauaji ya kinyama ya Wapalestina zaidi ya 100 yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza.
Amesema, "Shambulio dhidi ya shule ya Tabieen ni katika mfululizo wa hujuma za anga zinazofanywa na Israel dhidi ya majengo na makazi ya raia huko Gaza tangu vita vianze mapema Oktoba, 2023."
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa X kuwa: Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, kwa kutumia silaha za Marekani na Ulaya, mbele ya kimya cha mataifa yanayoitwa eti ya kistaarabu.
Jumamosi alfajiri, askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel walifanya "shambulio la kikatili ambalo halijawahi kushuhudiwa kwenye shule ya Tabieen inayowahifadhi wakimbizi huko Gaza, na kuua kwa umati Wapalestina zaidi ya 100.
Kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu jana Jumamosi iliripoti kuwa, mabomu yaliyotumiwa katika shambulio dhidi ya shule ya Tabieen yaliundwa na kusambazwa na Marekani.