Maafisa wa jeshi la Israel wamepoteza matumaini ya kupata ushindi katika vita vya Ghaza
Aug 12, 2024 03:08 UTC
Maafisa wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wamekiri kuwa, ushindi dhidi ya Muqawama wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza uko mbali sana kupatikana.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Jazeera maafisa wa jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza wamempelekea salamu Mkuu wa Majeshi ya Utawala huo Herzi Halevi wakikiri kwamba kutokana na hali inavyoendelea huko Ghaza ushindi katika vita uko mbali kupatikana.
Salamu za maafisa wa jeshi la Israel kwa Mkuu wa Majeshi ya utawala huo zimeeleza kwamba vita vya Ghaza vimeingia siku ya 310 huku wapiganaji wa Muqawama wakiwa wangali wanatoa vipigo vikali kwa wavamizi hao wa Kizayuni.
Vyombo vya habari vya Israel navyo pia vimeashiria hali inavyoendelea katika vita dhidi ya Ghaza na maafa wanayopata wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na kukiri kuwa, ahadi zilizotolewa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu katika kipindi cha miezi 10 iliyopita kuhusu kushinda vita hivyo na kuiangamiza Hamas ni za kuwahadaa watu tu.
Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth, hisia za kukata tamaa zinahisika ndani ya makao makuu ya jeshi la utawala wa Kizayuni kutokana na matatizo ambayo jeshi hilo linakabiliana nayo kwa kutokuwepo lengo la kisiasa linaloeleweka.
Baada ya kupita zaidi ya miezi 10 tangu utawala wa Kizayuni uuvamie kijeshi Ukanda wa Ghaza bila ya kupata mafanikio yoyote, utawala huo unazidi kuzama kwenye kinamasi cha migogoro yake ya ndani na nje siku baada ya siku.
Katika muda wote huo, utawala huo ghasibu haujafanikiwa katika lolote huko Ghaza zaidi ya kufanya mauaji ya halaiki, uharibifu, uhalifu wa kivita, ukiukaji wa sheria za kimataifa, uripuaji majengo ya mashirika ya utoaji misaada na kuwatesa kwa njaa Wapalestina wa eneo hilo.../