Kikao cha Baraza la Usalama kuhusu vita vya Ghaza; makabiliano ya Marekani na Jamii ya Kimataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen katika Ukanda wa Ghaza kilifanyika siku ya Jumanne ambapo akthari ya wanachama wa Baraza hilo walilaani jinai ya utawala huo na kusisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa vita mara moja huko Ghaza.
Wakati nchi nyingi, hata zile za Ulaya, zilichukua msimamo wa kuikosoa Israel, Marekani ilitosheka na kuonyesha kusikitishwa tu na mauaji ya kinyama ya Skuli ya Al-Tabeen, huku ikitilia mkazo mismamo wake wa kuendelea kuiunga mkono Tel Aviv.
Katika jinai ya karibuni zaidi liliyofanya alfajiri ya kuamkia siku ya Jumamosi, jeshi la utawala wa Kizayuni liliwashambulia kwa mabomu mazito Waislamu Wapalestina waliokuwa wakisali Sala ya Alfajiri katika Skuli ya Al-Tabeen iliyoko kwenye kitongoji cha Al-Daraj katika mji wa Ghaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 100 waliuawa shahidi na wengine wengi walijeruhiwa.
Wapalestina wapatao 200 waliolazimika kuhama makazi yao walikuwa wakisali Sala ya Alfajiri katika jengo la skuli hiyo walipoandamwa na shambulio la kinyama la jeshi la anga la utawala haramu wa Israel.
Jeshi la Kizayuni liliiteketeza Skuli ya Al-Tabeen kwa kutumia mabomu matatu, ambayo kila moja lilikuwa na uzito wa karibu kilo 500. Ikumbukwe kuwa, Marekani ndiyo iliyoupatia utawala wa Kizayuni makombora hayo.
Ofisi ya Habari ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza ilitangaza kuwa, Marekani na Israel kwa pamoja, ndizo zinazobeba dhima ya jinai hiyo ya kutisha. Utawala wa Kizayuni umedai kuwa jeshi lake liliwaua shahidi wanachama 19 wa makundi ya Muqawama katika hujuma hiyo ya anga, lakini Hamas na makundi mengine ya Muqawama yamekanusha vikali dai hilo.
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili shambulio dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen kiliitishwa kutokana na uzito na ukubwa wa unyama na ukatili uliofanywa na utawala wa Kizayuni, na namna ya uchinjaji na uteketezaji roho za watu uliofanywa na Israel na athari zake kwa mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano katika vita vya Ghaza.
Akihutubia kikao hicho, Rosemary DeCarlo, Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa na amani, aliashiria hali ya vita vya Ghaza na shambulio la Israel dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen na akasema: "hakuna sehemu yoyote ya Ghaza iliyo salama, lakini raia wangali wanaamrishwa wafunge virago kuhamia maeneo mengine, ambapo kila sehemu wanayokwenda inakuwa ndogo zaidi. Miezi 10 imepita tangu vilipoanza vita; na hatari ya kushadidi mvutano wa kikanda inahisika zaidi kuliko wakati wowote ule".
Katika kikao hicho cha Baraza la Usalama, msimamo wa wanachama wanne wa kudumu ulikuwa wa maana kulinganisha na wa Marekani kuhusiana na jinai za Israel. Linda Thomas Greenfield, balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, yeye alitosheka na kueleza tu kwamba, ametiwa wasiwasi na shambulio la Israel dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen huko Ghaza, na akadai kwamba, Washington imeibainishia Israel wasiwasi huo ilionao. Greenfield alisisitiza kuwa, nchi yake iko tayari kuulinda utawala wa Kizayuni na wanajeshi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati dhidi ya tishio lolote.
Kwa upande mwingine, balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa yeye alikumbusha kuwa, skuli 21 za Ukanda wa Ghaza zilizowapa hifadhi wakimbizi wa Kipalestina zimeshambuliwa kwa mabomu na utawala wa Kizayuni na akasisitiza kwamba, suala hilo linaonyesha kuwa Tel Aviv inayalenga kwa makusudi maeneo hayo yanayotoa hifadhi kwa raia wa Palestina.
Katika mkutano huo, mwakilishi wa China yeye alitoa wito wa kusitishwa mara moja harakati zote za kivita na za ujenzi wa vitongoji zinazofanywa na Israel na akalaani vikali shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen sambamba na kusisitiza kuwa miundombinu ya kiraia haipasi kulengwa na mashambulio ya kijeshi; na kwamba huo ni mstari mwekundu katika sheria za kimataifa za huduma za kibinadamu.
Suala muhimu lililoashiriwa na mwakilishi wa China ni kwamba Marekani imekuwa ikidai kuwa Israel imekubali makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini ukweli uko kinyume kabisa na hivyo. Badala ya kuonekana ishara madhubuti za kuthibitisha kwamba Israel imekubali kusitisha mapigano, kinachoonekana ni kupanuka kwa operesheni za kijeshi na kuongezeka kwa vifo vya raia.
Sambamba na hayo, Uingereza na Ufaransa nao pia zilionyesha msimamo hasi dhidi ya vitendo vya kijinai vya Israel huko Ghaza. Naibu Mwakilishi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa alisema unyanyasaji wa wafungwa wa Kipalestina na sera ya kudhikisha makusudi kwa njaa inayotumiwa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza ni jinai ya kivita na akaongeza kuwa, hakuna mahali palipo salama huko Ghaza kutokana na kutolewa agizo la kuhama ambalo limehusisha 86% ya eneo lote la ukanda huo.
Mwakilishi wa Ufaransa yeye pia alisema katika mkutano huo: "Ufaransa inalaani vikali shambulio la Israel katika Skuli ya Al-Tabeen huko Ghaza."
Suala jengine ni kwamba wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama, nao pia katika matamshi yao wamelaani hatua za utawala wa Kizayuni hususan shambulio dhidi ya Skuli ya Al-Tabeen na kutoa wito wa kusitishwa mara moja vita vya Ghaza.
Kutokana na yote hayo, kikao cha Baraza la Usalama kilichofanyika siku ya Jumanne kimedhihirisha kuwa, kuendelezwa jinai za utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi 11 ya vita vya Ghaza na mauaji ya kutisha yanayofanywa na utawala huo, ambayo yanaweza kutafsiriwa kama jinai za makusudi zinazowalenga wananchi madhulumu wa Ghaza hususan wanawake na watoto, sambamba na kutumia silaha ya kuwadhikisha na kuwaweka na njaa Wapalestina hao, ni masuala ambayo yameibua upinzani mkali wa Jamii ya Kimataifa dhidi ya Israel; na Marekani, ambayo ni mshirika wa kistratejia wa utawala huo wa Kizayuni inazidi kutengwa siku baada ya siku na kuzidi kubaki peke yake katika kuuunga mkono utawala huo wa kinyama.../