Bin Salman ahofia kuuawa kwa kufuatilia mpango wa kuanzishwa uhusiano rasmi kati ya Saudia na Israel
Aug 15, 2024 03:45 UTC
Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman ameripotiwa kuwa anahofia "kuuawa" kwa sababu ya juhudi zake za kutaka kuhakikisha ufalme huo unaanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Jarida la habari la mtandaoni la Politico la nchini Marekani limefichua suala hilo katika makala iliyochapishwa jana Jumatano, ikiashiria mazungumzo ya hivi karibuni aliyofanya Bin Salman na wabunge wa Wamarekani.
Sehemu ya makala hiyo ya Politico imedokeza kuwa Mwanamfalme huyo wa Saudia amewaambia wajumbe hao wa Kongresi ya Marekani kwamba anaweka maisha yake hatarini kwa kutaka kufikia makubaliano makubwa na Marekani na Israel ambayo ni pamoja na Saudia kuanzisha uhusiano rasmi na Israeli.
Politico limeendelea kufichua kuwa, "katika tukio moja, (Bin Salman) amemtaja kama mfano aliyekuwa rais wa Misri Anwar Sadat, aliyeuawa baada ya kufikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel, akiuliza nini Marekani ilifanya kumlinda Sadat".
Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2020, Muungano wa Falme za Kiarabu,UAE, Bahrain, Sudan, na Morocco zilisaini mikataba ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel kwa upatanishi wa Marekani.
Washington imeripotiwa kuwa inafanya juu chini kuiongeza Riyadh kwenye orodha hiyo ikiwa ni katika jitihada za kuifanya Tel Aviv, ambayo ni muitifaki wake mkuu, ipate uungaji mkono zaidi wa kikanda.
Lakini mnamo mwezi Septemba mwaka jana, utawala wa Kifalme wa Saudia uliripotiwa kuijulisha Marekani juu ya uamuzi wake wa kusimamisha mazungumzo yote yanayohusu uwezekano wa kukaribiana na Israel kwa madai kwamba baraza la mawaziri la utawala huo wa Kizayuni halitaki kufikia makubaliano yoyote na Wapalestina.
Pamoja na hayo, Politico limemnukuu afisa wa zamani wa Marekani na watu wengine wenye taarifa za mazungumzo kati ya Bin Salman na wajumbe wa Kongresi wakieleza kwamba mrithi huyo wa ufame wa Saudia anaonekana kuwa na nia ya kutekeleza mpango huo mkubwa na Marekani na Israel licha ya hatari iliyopo, kwa sababu anaiona hatua hiyo kuwa ni muhimu kwa mustakabali wa nchi yake kiusalama na kimaendeleo.../