HAMAS: Marekani ni mshirika wa Israel katika uhalifu wa kivita huko Gaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema Marekani ni mshirika wa muda mrefu wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza, na imeendelea kutoa uungaji mkono wake wa kisiasa, kijeshi na kiusalama kwa utawala huo ghasibu.
Hayo yamesemwa na Osama Hamdan, Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon katika mahojiano na kanali ya al-Jazeera ya lugha ya Kiarabu, ambapo amepinga mapendekezo mapya ya Washington akisema hayana lolote jipya, na kwamba yanalenga tu kuipa muda Israel wa kufanya uhalifu zaidi Gaza.
Ameeleza bayana kuwa, "Hakuna jipya isipokuwa kile tunachosikia kwenye vyombo vya habari na kile kinachojadiliwa na wapatanishi kuhusu nia ya Rais wa Marekani kuwasilisha pendekezo jipya."
Hamdan amesisitiza kuwa, ni wazi kwamba utawala wa Marekani kwa kiasi kikubwa umekuwa mshirika wa Israel katika jinai zake na mauaji ya halaiki yaliyofanywa huko Gaza.
Afisa wa ngazi ya juu wa HAMAS na ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya kundi hilo ameitaka Washington kumshinikiza Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa Julai 2, badala ya kutoa mapendekezo mapya.
Kwa mujibu wa Hamdan, kujiondoa kikamilifu kwa Israel kutoka eneo lote la Gaza, ikiwa ni pamoja na korido ya Philadelphi na usitishaji wa kudumu wa mapigano, ni sehemu ya makubaliano hayo na Muqawama hautarudi nyuma na utaendelea kupigania matakwa yake.