Vifo vya taratibu vya wakazi wa Ukanda wa Gaza kutokana na njaa kali
Mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza pia yamesababisha vifo vya taratibu kwa wakazi wa ukanda huo kutokana na njaa kali.
Mauaji hayo ya kimbari ya utawala wa Kizayuni yanakaribia kutimiza mwaka mmoja tangu tarehe 7 Oktoba, mwaka uliopita wakati utawala huo katili wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kila upande katika ukanda huo ambapo umedondosha karibu tani 80,000 za mabomu katika maeneo tofauti ya eneo hilo.
Kiasi hiki cha mabomu kinamaanisha kuwa, utawala wa Kizayuni umetumia kilo 36 za mabomu kuua kila mwanaume, mwanamke na mtoto wa Gaza.
Jinai hiyo si tu imepelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa watu wa Gaza, bali kwa hakika imening'iniza kivuli cha mauti kwenye vichwa vya watu wa ukanda huo ambapo maelfu ya watu waliojeruhiwa katika vita pia wanaendelea kupoteza maisha.
Aidha utawala dhalimu wa Israel na waziri mkuu wake mchinjaji Benjamin Netanyahu, wameibua mgogoro mkubwa wa njaa katika ukanda huu kwa kuzuia kutumwa huko misaada yoyote ya kibinadamu na hivyo kufanya njaa kuwa chombo muhimu cha kuwaua shahidi watu wa ukanda huu hasa wanawake na watoto. Adui Mzayuni anafuatilia kwa nguvu zake zote siasa za kuwanyima chakula ili kuwaua kwa njaa wakazi wa Gaza. Kuhusiana na suala hilo, Umoja wa Mataifa na taasisi zinazohusika nao zimetahadharisha kuhusu mzozo mkubwa wa njaa katika maeneo tofauti ya Gaza, mzozo ambao unasababisha ongezeko la vifo vinavyotokana na njaa, na kusisitiza kuwa zaidi ya watoto elfu 50 wa eneo hilo wanakabiliwa na utapiamlo mkali na kwamba hali hiyo mbaya ya kibinadamu ni zaidi ya maafa.
Víctor Aguayo, mkurugenzi wa kitengo cha lishe katika shirika la UNICEF, amesema kuwa zaidi ya watoto elfu 50 katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wanahitaji matibabu ya haraka. Amesema: "Tunakabiliwa na mlipuko unaokaribia mgogoro mkubwa wa kibinadamu na ongezeko la vifo vya watoto kutokana na njaa kali huko Gaza.' Watoto 9 kati ya 10 katika ukanda huu hawana virutubisho vya kutosha vya kudhamini ukuaji wao wa kiafya ambapo ongezeko kubwa la kiwango cha utapiamlo kati ya watoto na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha ni tishio kubwa kwa maisha yao."
Kwa upande mwingine, Stephan Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametoa onya kali na kusema kwamba zaidi ya watu milioni moja kusini na katikati mwa Gaza hawakupokea msaada wowote wa chakula mwezi uliopita wa Agosti.
Vifo vinavyotokana na njaa ni mfano mmoja tu wa unyama wa kutisha unaofanywa na utawala katili wa Israel dhidi ya watoto wa Gaza. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetoa onyo kali katika ripoti yake kuhusu uharibifu mkubwa wa kiakili na wa kisaikolojia unaosababishwa na utawala huo wa kibaguzi kwa watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa watoto hao wanasumbuliwa na viwango vya juu vya msongo wa mawazo. UNRWA vile vile imeripoti kuwa asilimia 90 ya watu wa Gaza wanahitajia moja kwa moja misaada ya nje ili kukidhi mahitaji yao ya chakula, na kuwa watoto ndio wanakabiliwa na hali mbaya zaidi ambapo wamekumbwa na upungufu mkubwa wa maji na utapiamlo. Catherine Russell, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, pia ameongeza kuwa; "Kiwango hiki cha vifo ambavyo tumevishuhudia katika Ukanda wa Gaza katika miezi michache iliyopita hakijawahi kutokea tena katika mzozo mwingine wowote wala mahala popote pale duniani."
Osama Hamdan, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), amesema: 'Adui Mzayuni amefunga vivuko vyote katika Ukanda wa Gaza na hivyo kufanya vifo vinavyotokanana na njaa kali katika ukanda huo kuwa ukweli mchungu usiokanushika. Utawala huo ghasibu na wa kifashisti ungali unaendeleza vita vya njaa kali dhidi ya wananchi wa Palestina huko Gaza ambapo watoto laki tatu na nusu walio chini ya umri wa miaka 5 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.