Sep 15, 2024 02:15 UTC
  • Kuafikiana makundi ya Kipalestina juu ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni

Kikao cha pande tatu kati ya harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Harakati ya Ukombozi ya Kiarabu na Harakati ya Ukombozi wa Palesetina kimefanyika na washiriki wa kikao hicho kusisitiza kuhusu haki ya wananchi wa Palestina ya kuendesha mapambano ya ukombozi dhidi ya maghasibu wa Kizayuni.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas)  Ijumaa Septemba 13 ilitangaza kuwa imefanya kikao cha pande tatu kati yake na Harakati ya Ukombozi ya Kiarabu na  Harakati ya Ukombozi wa Palestina huko Ukanda wa Gaza. Hamas imesisitiza katika taarifa yake kuwa haki ya wananchi wa Palestina ya kuendesha mapambano dhidi ya maghasibu ni haki yao kisheria kwa njia yoyote ile; haki ambayo haipasi kutiliwa shaka au kukandamizwa. Makundi hayo matatu pia yamesisitiza kuwa wananchi wa Palestina pamoja na vikosi vya kitaifa ni raia ambao wanapaswa kujianishia mustakbali wao wenyewe na kuchukua maamuzi kuhusu hatima yao baada ya vita. 

Makundi hayo pia yametilia mkazo na kuhimiza kuhusu ulazima wa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo ili kutekeleza mapatano ya umoja wa kitaifa yaliyofikiwa huko Beijing na yale ya kabla yake, na kuwepo ulazima wa kurejesha itibari ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina na kuifanyia marekebisho ili kuifanya kuwa nyumba ya Palestina ambayo inawaleta pamoja raia wote wa Palestina.

Harakati ya Hamas 

Mwezi Julai 2024, wawakilishi wa makundi 14 na mirengo ya kisiasa ya Palestina ikiwa ni pamoja na Fat'h na Hamas walisaini mapatano ya awali kwa ajili ya kuasisi serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa baada ya siku tatu za mazungumzo makubwa huko Beijing. Taarifa ya mwisho ya kikao hicho iliyokuwa na vipengee nane ilisisitiza kuhusu haki ya wananchi wa Palestina na kuendesha muqawama dhidi ya maghasibu wa Kizayuni na kuhitimisha hatua za ukaliaji mabavu kwa mujibu wa sheria zote za kimataifa na mkataba wa Umoja wa Mataifa na kurejea  Wapalestina katika ardhi zao kwa mujibu wa azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  

Kikao cha pande tatu cha Septemba 13 mwaka huu kati ya makundi ya Palestina huko Gaza kinaashiria kuanza duru mpya ya jitihada za makundi hayo kwa ajili ya kuandaa nyanja za ushirikiano na mshikamano zaidi kwa lengo la kukabiliana na hatua haribifu za Wazayuni na muungaji mkono wao mkuu Marekani katika eneo. Washington na Tel Aviv zinaendeleza chokochoko na kuibua mivutano bila ya kutilia maanani hali ya mambo katika eneo na kwa lengo la kukabiliana na mhimili wa muqawama.  

Tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza; viongozi wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wameainisha mipango yao mingi ya njozi na isiyo na msingi mkabala wa mustakbali wa ukanda huo, na katika wakati fulani waliazimia kutekeleza mipango yao hiyo miovu hata kabla ya kumalizika vita vya Gaza lakini hakuna hata mmoja uliofanikiwa.

Mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza 

Hamas ina nafasi athirifu katika matukio ya Palestina na katika eneo kwa ujumla; na malengo maovu ya Wazayuni yatagonga mwamba kwa kuzingatia uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa harakati hiyo. Kikao cha Gaza kinaonyesha azma thabiti ya makundi ya Palestina kwa ajili ya umoja na kushikamana pakubwa na wakati huo huo kinasisitiza kuhusu stratejia ya muqawama katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Matukio ya Gaza yanaonyesha kuwa makundi ya mapambano ya Palestina yanasisitiza kutekelezwa mpango jumuishi wa Wapalestina kwa ajili ya mustakabali wa nchi yao bila ya uingiliaji kati wa maajinabi.  

Kuwepo uratibu na kuungana makundi ya muqawama ya Palestina, licha ya kuendelea  vita dhidi ya Gaza, kutaifanya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi kwa utawala wa Kizayuni kuliko hapo awali, na kuyawezesha makundi ya mapambano kufanikisha malengo na mipango yao. 

Kuendesha mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na kutambuliwa haki halali za wananchi wa Palestina ni stratejia kuu ya makundi ya mapambano ya Palestina ambayo yanasisitiza juu ya kupatikana haki hizo.