Sep 15, 2024 11:41 UTC
  • Israel yaajiri Waafrika wanaotafuta hifadhi kwa ajili ya kupigana vita dhidi ya watu wa Gaza

Gazeti la Israel la Haaretz limefichua kuwa, Israel inawaajiri wahajiri kutoka Afrika kama sehemu ya operesheni zake za kijeshi katika vita vya utawala huo kaktili dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, mkabala wa kuwapa haki za ukaazi.

Gazeti hilo limewanukuu maafisa wa serikali wakisema kuwa, jeshi la Israel "linawasaidia watafuta hifadhi Waafrika wanaochangia katika vita huko Gaza na kuhatarisha maisha yao, ili kupata hati ya ukaaji wa kudumu katika utawala huo wa Israel."

Maafisa wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel, ambao wamezungumza kwa njia isiyo rasmi na gazeti la Haaretz, wamesema kuwa mradi huo unaendelea kwa utaratibu maalumu, chini ya uongozi wa washauri wa kisheria wa jeshi, lakini bila kuzingatia kipengele cha maadili cha kuajiri waomba hifadhi hao wa Kiafrika.

Ripoti ya gazeti hilo inasema, hadi sasa hakuna hata mmoja wa waomba hifadhi wa Kiafrika walioshiriki katika vita hivyo ambaye amepewa hadhi rasmi.

Kwa sasa waomba hifadhi wapatao 30,000 wa Kiafrika, ambao wengi wao ni vijana, wanaishi Israel, na Wasudani wapatao 3,500 wamepewa hadhi ya muda iliyotolewa na mamlaka ya mahakama, wakisubiri uamuzi wa maombi yao ya ukaazi.

Israel imeendelea kupuuza maamuzi ya jamii ya kimataifa, hususan azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusimamisha vita mara moja Ukanda wa Gaza, na hadi sasa imeua karibu raia elfu 50 wa Kipalestina katika eneo hilo.