Shambulio la Yemen Tel Aviv; onyo kali la Mhimili wa Muqawama kwa utawala wa Kizayuni
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameitaja oparesheni ya makombora ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya Tel Aviv kuwa ni la aina yake kuwahi kufanywa katika historia ya adui mvamizi Israel.
Vyombo vya habari jana vilitangaza taarifa ya kuvurumishwa kombora karibu na Tel Aviv mji mkuu wa utawala wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuzuka moto baada ya kurushwa kombora hilo. Kufuatia shambulio hilo la kombora, kengele za hatari zilisikika katikati ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu katika karibu miji na vitongoji 20 mashariki na kusini mwa Tel Aviv.
Shirika la habari la IRNA limetangaza kuwa, Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameweka wazi shambulio hilo la kombora kuelekea Tel Aviv na kusema: Oparesheni hiyo ilifanywa na kombora jipya la balistiki la Hypersonic na mifumo ya ulinzi ya utawala wa kizayuni imeshindwa kukabiliana na kulizuia kombora hilo.
Saree amesisitiza kuwa kombora hilo jipya la balistiki la Hypersonic lilirushwa hadi Tel Aviv kwa kutumia muda wa dakika 11 na sekunde 30 katika umbali wa kilomita 2040; jambo lililowatia kiwewe na hofu Wazayuni na kupelekea Wazayuni zaidi ya milioni mbili kukimbilia mafichoni.
Naye Mohammed al Atifi Waziri wa Ulinzi wa Yemen juzi aliuonya muungano wa Marekani na Uingereza na kusema katika siku zijazo adui Mzayuni atakabiliwa na mshangao ambao hakuutarajia.