Sep 17, 2024 02:27 UTC
  • Kombora la jeshi la Yemen dhidi ya Tel Aviv; kushindwa kukubwa kwa ulinzi wa anga wa utawala wa Kizayuni

Ikiwa ni katika kuendelea kuwatetea wananchi wa Ukanda wa Gaza dhidi ya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni, Harakati ya Ansarullah ya Yemeni imelenga mji wa Tel Aviv kwa kombora la balistiki ambapo mifumo ya ulinzi wa anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeshindwa kuzuia kombora hilo.

Jumapili asubuhi, vyanzo vya habari viliripoti kwamba kombora la Yemen lilipiga eneo la karibu na Tel Aviv na moto ukazuka baada ya hapo. Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa Jeshi la Yemen, huku akifafanua operesheni hiyo ya kipekee ya kombora amesema kuwa tukio hilo limetokea kwa mara ya kwanza katika historia bandia ya adui Mzayuni. Amesema katika taarifa kwamba operesheni hiyo dhidi ya Tel Aviv ambayo imefanywa kwa kombora jipya la balistiki la Hypersonic, imefikia lengo lake na kwamba mifumo ya ulinzi ya adui alishindwa kulizuia. Ameongeza kuwa kombora hilo lilisafiri umbali wa kilomita 2,040 kwa muda wa dakika 11 na sekunde 30, ambapo liliwasababishia Wazayuni kiwewe na hofu kubwa na kupelekea zaidi ya milioni mbili kati yao kukimbilia mafichoni chini ya ardhi, na kuwa tukio hilo lilikuwa la kwanza kutokea katika historia ya Wazayuni.

Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen

Kwa kutilia maanani matamshi hayo ya msemaji wa Jeshi la Yemen, tanapasa kuashiria hapa nukta hii kuwa operesheni ya Jumapili imethibitisha wazi kwamba Wayemen wamefikia teknolojia na ujuzi mkubwa wa kijeshi wa kutengeneza kombora la Hypersonic na hivyo kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo kwa manufaa ya mhimili wa muqawama ambapo haya yote yamepatikana licha ya vita na vikwazo vya miaka 9 na mzingiro wa kiuchumi wa maadui dhidi ya taifa la Yemen.

Nukta nyingine muhimu kuhusu operesheni ya Jumapili ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ni kutokuwa na uwezo wa mfumo wa ulinzi wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kulizuia kombora hilo. Wayemen walirusha kombora moja tu kuelekea Tel Aviv, ambalo lilisafiri umbali wa kilomita 2,040 bila kuzuiliwa. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, kombora hilo lilipiga njia ya reli ya Tel Aviv kuelekea Quds Tukufu, karibu kilomita 6 kutoka mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Sayyid Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah amesema kuhusiana na suala hilo kwamba operesheni ya Jumapili ilifanywa kwa kombora la hali ya juu kabisa, kusafiri umbali wa kilomita 2,040 na kukwepa mifumo ya ulinzi ya adui kwa mafanikio makubwa.

Operesheni ya Jumapili ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeanika wazi udhaifu mkubwa wa utawala wa Kizayuni. Vyanzo vya Kizayuni vimesema kuwa, ijapokuwa shambulio la  Yemen lilitekelezwa kwa kombora moja tu, lakini lilipelekea idadi kubwa ya wakaazi wa mji mkuu na miji ya jirani kukimbilia mafichoni. Hivyo, ukosefu wa usalama na hofu kwa walowezi wa ardhi za Palestina imeangaziwa tena kwa kiwango kikubwa.

Yemen yaipiga Tel Aviv kwa kombora lake jipya la balistiki 

Suala jingine ni kwamba operesheni ya kombora ya jeshi la Yemen huko Tel Aviv imeanika wazi udhaifu mkubwa wa mifumo ya ulinzi ya majini ya Marekani na Uingereza katika eneo muhimu la Bab al-Mandab, Bahari Nyekundu na Mediterania. Marekani na Uingereza zimeongeza uwepo wao katika maeneo hayo katika miezi ya karibuni, na kama  Sayyid Abdul Malik al-Houthi alivyosema, nchi hizo zimefanya zaidi ya mashambulio 700 ya makombora dhidi ya Wayemen, lakini pamoja hayo sio tu suala hilo halijapunguza uwezo wa Wayemen kufanya mashambulizi dhidi ya adui, bali  hata limewapelekea kufanya operesheni kubwa ya kombora na ya kipekee dhidi ya Tel Aviv.

Nukta nyingine muhimu ni kuwa Wayemen wamefanya shambulizi hilo la kombora dhidi ya Tel Aviv katika kuwaunga mkono watu wa Ukanda wa Gaza wanaoendelea kuuawa kwa umati na Utawala katili wa Israel, na hii ndio maana kombora hilo likapewa jina la "Palestina nambari 2". Yemen ndio nchi na jeshi pekee la Kiarabu ambalo limewatetea watu wa Gaza katika mwaka mmoja uliopita, wakati utawala wa Kizayuni unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza, na uungaji mkono huo bila shaka utaendelea kuwepo hadi pale Wazayuni watakapoacha kufanya mashambulizi ya kinyama katika ukanda huo. Sayyid Abdul Malik al-Houthi amesema: "Kadiri uvamizi na mzingiro wa Ukanda wa Gaza unavyoendelea, operesheni zetu nazo zitaendelea. Msimamo wetu utaendelea kuwa imara hadi kukombolewa ardhi zote za Palestina kutoka mikononi mwa uvamizi. Tutaendelea kuratibu mambo yetu na mhimili wa jihadi na muqawama, na yale yaliyoko njiani ni makubwa zaidi ya haya mnayoona."

Jambo la mwisho muhimu ni kuwa mashambulio ya Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni yanatekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa wananchi wa nchi hiyo. Dalili ya uungaji mkono huo ni mahudhurio makubwa ya mamilioni ya Wayemen kutoka mikoa mbalimbali ya nchi katika Maulidi ya Mtume Muhammad (saw). Uungaji mkono huo wa wananchi bila shaka unaimarisha azma ya jeshi la Yemen ya kuendelea kuwaunga mkono watu wa Ukanda wa  Gaza na kutowaogopa maadui Wazayuni na Wamarekani.

Tags