Kinyume na uongo wa Netanyahu, UN yasema: Israel imezuia 90% ya misaada ya kuingizwa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i116866-kinyume_na_uongo_wa_netanyahu_un_yasema_israel_imezuia_90_ya_misaada_ya_kuingizwa_ghaza
Umoja wa Mataifa umesema, kuna changamoto kadhaa zinazokabili shughuli za ufikishaji misaada ya kibinadamu kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Ghaza, na kubainisha kuwa 90% ya misaada hiyo iliyokuwa imeratibiwa kufikishwa kwenye maeneo hayo ama imekataliwa au kuzuiliwa hadi sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mwezi huu wa Septemba.
(last modified 2024-09-28T06:33:57+00:00 )
Sep 28, 2024 06:33 UTC
  • Kinyume na uongo wa Netanyahu, UN yasema: Israel imezuia 90% ya misaada ya kuingizwa Ghaza

Umoja wa Mataifa umesema, kuna changamoto kadhaa zinazokabili shughuli za ufikishaji misaada ya kibinadamu kaskazini na kusini mwa Ukanda wa Ghaza, na kubainisha kuwa 90% ya misaada hiyo iliyokuwa imeratibiwa kufikishwa kwenye maeneo hayo ama imekataliwa au kuzuiliwa hadi sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mwezi huu wa Septemba.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, shughuli za ufikishaji misaada ya kibinadamu huko Ghaza zinaendelea kukabiliwa na vikwazo vikubwa.
 
"Takribani 90% ya shughuli za kibinadamu zilizoratibiwa kufikishwa kaskazini na kusini mwa Ghaza hadi sasa katika mwezi Septemba zimekataliwa au kuzuiwa," amesema Dujarric.
 
Msemaji huyo wa UN amebainisha pia kuwa idadi ya vikwazo vya ndani ilivyowekwa na vikosi vya Israel dhidi ya shughuli za ufikishaji msaada iliongezeka kwa zaidi ya 20% tangu Juni 2023.
Stephane Dujarric

Aidha, Dujarric ametoa indhari kuwa, watu huko Ghaza wanaendelea kuishi katika hali mbaya ambayo inaweza kuharibika na kuwa mbaya zaidi katika hali ya hewa ya baridi na mvua ya msimu unaokaribia wa baridi kali.

 
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa hiyo kuhusu kukataliwa na kukwamishwa asilimia 90 ya misaada inayokusudiwa kupelekwa kwa Wapalestina wa Ghaza katika hali ambayo, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alidai alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa kwamba, utawala huo unaruhusu kwa kiwango kinachostahiki kuingizwa misaada katika eneo hilo uliloliwekea mzingiro.

Utawala dhalimu wa Kizayuni ungali unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza ulivyoanzishwa Oktoba 7 mwaka jana licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika eneo hilo.

Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 41,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na zaidi ya 96,000 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza.

Mashambulizi ya kinyama ya Israel yamewafanya karibu wakazi wote wa Ghaza kuwa wakimbizi kutokana na mzingiro unaoendelea ambao umesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa.

Ikumbukwe kuwa, utawala wa Kizayuni unakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa vitendo vya kinyama unavyoendeleza huko Ghaza.../