Duru iliyo karibu na Hizbullah: Mwili wa Shahidi Sayyid Nasrullah umezikwa kwa muda 'sehemu isiyojulikana'
Oct 04, 2024 10:24 UTC
Duru iliyo karibu na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa mwili wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah umezikwa kwa muda katika sehemu isiyojulikana.
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu mashuhuri wa Hizbullah, ambaye aliongoza Mhimili wenye nguvu zaidi wa Muqawama katika eneo kwa muda wa miaka 32, hatimaye alifikia daraja tukufu na ya juu zaidi ya kufa shahidi kufuatia unyama na ukatili uliofanywa na Wazayuni.
Kufuatia tukio hilo, sasa hivi vyombo vya habari vimekuwa vikidadisi na kukisia kuhusu mahali na wakati wa kuzikwa kwa Sayyid huyo mtukufu.
Wakati baadhi ya vyanzo vimedai kuwa mwili wa Sayyid Hassan Nasrullah utahamishiwa Iraq na kuzikwa katika mji mtakatifu wa Karbala baada ya shughuli ya kuuaga itakayofanyika mjini Beirut Lebanon, hivi sasa viongozi wa Hizbullah wanakanusha uvumi huo.
Duru moja iliyo karibu na harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon imelitaarifu shirika la habari la AFP leo Ijumaa kwamba, kwa sababu ya ugumu wa kufanya shughuli ya maziko ya hadhara "kutokana na vitisho vya Israel", mwili wa Shahidi Sayyid Nasrullah "umezikwa kwa muda" mahali pasipojulikana.
Duru hiyo ambayo haikutaka kuweka wazi utambulisho wake, imesema: kutokana na hofu ya vitisho vilivyotolewa na Israel vya kuwalenga waombolezaji, mahali itakapofanyika shughuli ya kuuaga mwili na mahali pa maziko, "mwili wa Shahidi Nasrullah umezikwa kwa muda mahali pasipojulikana" hadi wakati muafaka ambapo shughuli ya mazishi itafanyika hadharani kwa kuwashirikisha watu wote.../