Malengo ya utawala wa Kizayuni katika hatua yake mpya dhidi ya UNRWA
Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA imekabiliwa na radiamali kali za kimataifa.
Bunge la utawala haramu wa Kizayuni, Knesset siku ya Jumatatu liliidhinisha sheria inayopiga marufuku shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Rasimu ya sheria hiyo ilipitishwa kwa kura 92 za ndio na 10 za hapana. Kwa kupitishwa sheria hiyo, makubaliano ya mwaka 1967 ambayo yaliruhusu UNRWA kufanya kazi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yatafutiliwa mbali, hivyo shughuli zote za shirika hilo zitasitishwa na mawasiliano yoyote kati ya maafisa wa Kizayuni na wafanyakazi wa UNRWA kupigwa marufuku.
UNRWA ilianzishwa mwaka 1949 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina katika nchi nyingi. Shirika hili ndilo mhimili wa usambazaji wa misaada ya kimataifa katika Ukanda wa Gaza, ambao sasa unakabiliwa na janga la kibinadamu lililosababishwa na jinai za kinyama za utawala huo dhidi ya wakazi wa ukanda huo.
Kwa kupitisha sheria hii, utawala wa Kizayuni unafuatilia malengo mawili makuu. Lengo la kwanza ni kuwawekea mashinikizo makali wananchi wa Ukanda wa Gaza ili wachukue hatua hasimu dhidi ya Hamas, wananchi ambao licha ya kukabiliwa na jinai za kikatili za utawala huo katika kipindi cha miezi 13 iliyopita, lakini bado wanauinga mkono Hamas kwa nguvu zao zote. Kwa hakika kupasishwa sheria hii ni muendelezo wa jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi na wanaharakati shupavu wa muqawama huko Gaza.
Lengo la pili ni kwamba, utawala wa Kizayuni kwa kupitisha sheria hii unaendelea kuuwekea mashinikizo Umoja wa Mataifa. Kwa hakika, hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni sehemu ya vita na uhasama wa utawala huo dhidi ya Umoja wa Mataifa. Katika mwaka mmoja uliopita, wakati wa vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza, utawala wa Kizayuni umezidisha makabiliano yake ya kiuadui dhidi ya Umoja wa Mataifa na taasisi zinazofungamana nao.
Kuhusiana na suala hilo watawala wa Kizayuni wamemtaja Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa mtu asiyetakiwa na kumpiga marufuku kukanyaga katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu huko Palestina. Umeshambulia mara kadhaa kwa mabomu makao ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNIFIL) na kuwataka kuhama eneo hilo. Mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa karibuni alichanachana Hati ya Umoja wa Mataifa kama alama ya matusi na dharau kwa umoja huo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, utawala wa Kizayuni umelenga mara nyingi vituo vya UNRWA na kuwaua kwa umati zaidi ya wafanyakazi wake 230.
Vitendo vya uhasama vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Umoja wa Mataifa vinatekelezwa katika hali ambayo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, shirika hilo limeshindwa kabisa kuchukua hatua yoyote ya maana ya kukomesha mauaji ya kimbari ya utawala huo huko Gaza. Pamoja na hayo, utawala huo wa kidhalimu hauvumilii hata kuona ukikosolewa kwa maneno matupu tu na maafisa wa Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yanayofungamana nao.
Hatua hiyo ya kibabe ya utawala wa Kizayuni imekabiliwa na ukosolewaji mkali katika ngazi za kimataifa, ambapo viongozi wa nchi tofauti za ulimwengu wamelaani kitendo hicho cha dharau cha utawala wa Kizayuni dhidi ya Umoja wa Mataifa. Viongozi wa nchi mbalimbali za dunia zikiwemo baadhi ya nchi za Ulaya wamesema kuwa, hatua ya bunge la Kizayuni ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA ni hatua hatari ambayo inaweza kuziathiri pia taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa katika maeneo mengine ya dunia, na wakati huo huo, kuongeza maafa ya kibinadamu huko Gaza. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza kuwa, kupitishwa sheria ya kupiga marufuku shughuli za shirika la UNRWA katika bunge la Kizayuni ni jambo lisilokubalika na kuwa litakuwa na matokeo mabaya sana kwa wakimbizi wa Kipalestina.