Gazeti la Kiebrania la Haaretz: Israel imeidhinisha mpango wa kuondoa askari wake Ukanda wa Ghaza
Jan 13, 2025 03:26 UTC
Gazeti la Kiebrania la Haaretz limeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeidhinisha mipango ya kuwaondoa wanajeshi katika Ukanda wa Ghaza, baada ya hatua zilizopigwa katika mazungumzo ya kubadilishana mateka na harakati ya Hamas.
Kwa mujibu wa Haaretz jeshi la Israel limeidhinisha mipango kadhaa ya kuwaondoa haraka wanajeshi kutoka Ghaza kama jibu kwa hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo.
Imeelezwa kuwa, jeshi hilo limechunguza machaguo kadhaa ya hatua za kuchukua, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wanajeshi katika Ukanda wa Netzarim, ambao unaigawanya Ghaza sehemu mbili.
Haaretz limeripoti kuwa, japokuwa jeshi la utawala wa Kizayuni lilikuwa limeshaanzisha miundombinu mingi na ngome kadhaa katika eneo hilo, lakini limesema linaweza "kuwahamisha" askari, likisisitiza utayari wake wa kutekeleza makubaliano yoyote yatakayofikiwa kati ya utawala huo na harakati ya Muqawama ya Palestina ya Hamas, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa haraka wanajeshi kutoka Ghaza.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel iliripoti hapo awali kwamba ujumbe wa utawala huo, ukiongozwa na Mkuu wa Mossad David Barnea na mkuu wa idara ya usalama wa ndani ya Shin Bet, Ronen Bar umesafiri kuelekea Qatar ili kuendelea na mazungumzo.
Kabla ya kutolewa tangazo hilo, Benjamin Netanyahu alikutana na Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump wa masuala ya Mashariki ya Kati.
Nalo gazeti la Yedioth Ahronoth limezinukuu duru za kisiasa na kuripoti kwamba 90% ya makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas yameshakamilika.../
Tags