HAMAS kuwaachia askari 4 wanawake wa Israel kwa Wapalestina 200 akiwemo kamanda wa Muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121878-hamas_kuwaachia_askari_4_wanawake_wa_israel_kwa_wapalestina_200_akiwemo_kamanda_wa_muqawama
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kamanda maarufu wa Palestina ataachiliwa leo ikiwa ni sehemu ya mabadilishano ya pili ya wafungwa na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya usitishaji vita katika Ukanda wa Ghaza kuanza kutekelezwa wiki iliyopita.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jan 25, 2025 03:09 UTC
  • HAMAS kuwaachia askari 4 wanawake wa Israel kwa Wapalestina 200 akiwemo kamanda wa Muqawama

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kamanda maarufu wa Palestina ataachiliwa leo ikiwa ni sehemu ya mabadilishano ya pili ya wafungwa na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya usitishaji vita katika Ukanda wa Ghaza kuanza kutekelezwa wiki iliyopita.

Abu Obeida, msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za al-Qassam, amesema mabadilishano ya pili ya wafungwa yanafanyika leo Jumamosi kama sehemu ya mapatano ya kusitisha mapigano na utawala wa Kizayuni ambayo yalianza kutekelezwa siku ya Jumapili iliyopita.
 
Aidha, ametangaza majina ya wanajeshi wanne wanawake wa Israel ambao Hamas itawaachia huru, nao ni Karina Araiv, Daniella Gilboa, Naama Levy, na Liri Elbaz.
 
Utawala wa Kizayuni umekubali kuwaachia huru wafungwa 50 Wapalestina kwa kila askari wake mmoja wa kike.
 
Kwa mujibu wa msemaji wa Al-Qassam, miongoni mwa Wapalestina 200 ambao utawala haramu wa Israel unapaswa kuwaachilia huru leo ni Zakaria Zubeidi, kamanda wa zamani wa muungano wa Muqawama wa Brigedi za Mashahidi wa al-Aqsa katika mji wa Jenin kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Abu Obeida amemtaja Zubeidi kuwa ni mmoja wa wafungwa wa Kipalestina, ambaye alitekeleza operesheni ya kihistoria ya kutoroka gereza la Gilboa la utawala wa wa Kizayuni wa Israel mwaka 2021 kwa kutumia vijiko tu kuchimba shimo kwenye sakafu ya gereza hilo.

Mfungwa huyo anatambuliwa pia kama nembo ya Intifadha ya Pili ya Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Kwa mujibu wa Abu Obeida, askari wa jeshi la Kizayuni walivamia nyumba ya Zakaria Zubeidi katika kambi ya wakimbizi ya Jenin kufuatia taarifa za kuwepo matarajio ya yeye kuachiliwa huru, wakampiga na kumfunga mkewe na watoto wake.../