Mkuu wa Hizbullah: Lebanon haitasahau msaada wa Iran, Iraq wakati wa vita vya Israel
-
Sheikh Naim Qassem
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, watu wa Lebanon hawatasahau uungaji mkono na msaada mkubwa waliopewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq wakati wa mashambulizi makali ya anga na nchi kavu ya Israel dhidi ya nchi yao.
Sheikh Naim Qassem ameyasema hayo katika hotuba yake iliyorushwa hewani moja kwa moja kwa njia ya televisheni kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut, jioni ya jana Jumatatu.
"Ushindi wa Gaza ni wa watu wa Palestina, mataifa ya kikanda yaliyowaunga mkono pamoja na watu wote wanaopigania uhuru kote duniani," amesema Sheikh Naim Qassem.
Mkuu huyo wa Hizbullah ameendelea kusema kuwa, njama za Israel zenye lengo la kuangamiza harakati ya Muqawama ya Hamas huko Palestina zimefeli vibaya na kufichua udhaifu wa utawala wa Tel Aviv. Amesema: "Adui Mzayuni hangeweza kuendelea kuwepo kwa wiki moja bila msaada usio na kikomo wa Marekani."
Sheikh Qassem amesisitiza kuwa, Muqawama na mapambano ndio chaguo la kisiasa, kitaifa na kibinadamu la kukabiliana na uvamizi wa Israel na kukomboa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Amesema malengo ya Operesheni kubwa ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyoanzishwa na harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina za Gaza dhidi ya utawala dhalimu wa Israel mnamo Oktoba 7, 2023, yamefikiwa.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: Adui, Israel, alishindwa mtihani wa heshima na ubinadamu na kuwa chombo cha uhalifu kinachofanya kazi ya kuangamiza wanadamu. "Israel imedhihirika kama mhalifu wa kivita na imeshindwa kukomboa mateka wake kwa njia yoyote ile isipokuwa kwa makubaliano na Hamas,” amesisitiza kiongozi wa Hizbullah.
Sheikh Naim Qassem ameyataja mashambulio ya Israel dhidi ya Lebanon na Ukanda wa Gaza kuwa ni vitendo vya ukatili vilivyoungwa mkono bila masharti na Marekani na baadhi ya serikali za nchi za Magharibi.