Jeshi la Israel laendelea kukalia maeneo ya ardhi ya Lebanon licha ya muhula wa kuondoka kumalizika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i122896
Muhula wa mwisho uliokuwa umetolewa kwa askari wote wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka kusini mwa Lebanon chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya utawala huo na harakati ya Hizbullah ulimalizika leo Jumanne, huku Israel ikitangaza kuwa itaendelea kubaki katika "maeneo matano ya kimkakati" ya ardhi ya nchi hiyo.
(last modified 2025-02-18T13:42:26+00:00 )
Feb 18, 2025 13:42 UTC
  • Jeshi la Israel laendelea kukalia maeneo ya ardhi ya Lebanon licha ya muhula wa kuondoka kumalizika

Muhula wa mwisho uliokuwa umetolewa kwa askari wote wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka kusini mwa Lebanon chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya utawala huo na harakati ya Hizbullah ulimalizika leo Jumanne, huku Israel ikitangaza kuwa itaendelea kubaki katika "maeneo matano ya kimkakati" ya ardhi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa Novemba 27, 2024 kwa usimamizi wa Marekani na Ufaransa, ilipangwa kuwa askari wa jeshi la Lebanon pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa watatumwa kushika udhibiti wa maeneo ya ardhi ya nchi hiyo sambamba na jeshi la Israel kujiondoa kwenye maeneo hayo ndani ya muda wa siku 60 ambao ulirefushwa hadi Februari 18.

Hata hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel umeviamuru vikosi vyake kubaki katika maeneo matano ya kistratejia kusini mwa Lebanon kinyume na mapatano hayo na licha ya indhari iliyotolewa na Hizbullah kwamba utawala huo ghasibu unakiuka makubaliano hayo.

Msemaji wa jeshi la Kizayuni Nadav Shoshani alitangaza jana: "wanajeshi wa Israel, kwa wakati huu, wanasalia katika vituo vya ulinzi ndani ya Lebanon "ili tuweze kuendelea kuwalinda wakazi wetu na kuhakikisha kuwa hakuna tishio la haraka". 

Duru moja ya Lebanon imeripoti kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni limejiondoa katika vijiji vyote vya mpakani isipokuwa katika vituo vitano, huku jeshi la Lebanon likiendelea kusonga mbele taratibu na kwa hali ya tahadhari kutokana na kuwepo mada za miripuko zilizoachwa na jeshi hilo katika baadhi ya maeneo na uharibifu wa barabara liliofanya katika maeneo hayo.

Kusini na mashariki mwa Lebanon pamoja na kusini mwa Beirut ni maeneo yaliyoshuhudia uharibifu mkubwa wakati wa miezi miwili ya vita vya kikatili na vya pande zote vilivyoanziishwa na utawala wa Kizayuni mwaka mmoja baada ya kuanzisha vita dhidi ya Ghaza.

Mamlaka za Lebanon zinakadiria gharama za ujenzi mpya wa maeneo yaliyoharibiwa kwa mashambulio ya jeshi la Kizayuni zinaweza kufikia zaidi ya dola bilioni 10, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionyesha kuwa raia zaidi ya 100,000 wamebaki kuwa wakimbizi wa ndani.

Aidha, watu 60 wameripotiwa kuuawa ndani ya Lebanon kutokana na mashambulio yaliyoendelea kufanywa na jeshi la Israel tangu yalipoanza kutekelezwa makubaliano ya usitishaji vita.../