UN: Mashambulio 36 ya Israel Ghaza kati ya Machi 18 hadi Aprili 9 yameua wanawake na watoto tu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i125058
Umoja wa Mataifa umesema wanawake na watoto wa Kipalestina ndio pekee waliouawa katika mashambulizi yapatayo 36 ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu katikati ya mwezi Machi na kuonya kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Israel yanahatarisha "kuendelea kuwepo Wapalestina kama jamii".
(last modified 2025-07-15T18:01:36+00:00 )
Apr 12, 2025 03:08 UTC
  • UN: Mashambulio 36 ya Israel Ghaza kati ya Machi 18 hadi Aprili 9 yameua wanawake na watoto tu

Umoja wa Mataifa umesema wanawake na watoto wa Kipalestina ndio pekee waliouawa katika mashambulizi yapatayo 36 ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu katikati ya mwezi Machi na kuonya kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Israel yanahatarisha "kuendelea kuwepo Wapalestina kama jamii".

Ravina Shamdasani, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza hayo na kufafanua kuwa ofisi hiyo ilirekodi mashambulizi 224 yaliyofanywa na jeshi la Israel dhidi ya majengo ya makazi na mahema ya watu waliolazimika kuhama makazi yao katika Ukanda wa Ghaza kati ya Machi 18 na Aprili 9.

"Katika mashambulizi 36 ambayo Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilithibitisha taarifa zake, vifo vilivyorekodiwa kufikia sasa ni vya wanawake na watoto tu", ameeleza Shamdasani.

Taarifa ya uchunguzi huo imetolewa wakati mashambulizi mapya ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza hadi sasa yameshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 1,500 tangu jeshi la utawala huo ghasibu livunje makubaliano ya usitishaji vita Machi 18.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeweka vizuizi kamili kwenye eneo la pwani ya Palestina na kuzuia kuingizwa kitu chochote ndani ya Ghaza, na kupelekea Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu kuonya kwamba chakula, maji, dawa na vifaa vingine muhimu vinamalizika haraka katika eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alitangaza kuwa, “zaidi ya mwezi mzima umepita bila ya hata tone moja la msaada kufika Ghaza”.

Guterres alilitaja eneo la Ukanda wa Ghaza lililowekewa mzingiro na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni “uwanja wa mauaji,” na akatoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja na kwa sura ya kudumu na kuruhusiwa misaada ya kibinadamu kuingizwa kwenye eneo hilo bila vizuizi.../