Kwa mara nyingine Yemen yayatwanga maeneo ya jeshi la Israel huko Jaffa
Jeshi la Yemen (YAF) limetangaza habari ya kufanya operesheni nyingine ya ndege zisizo na rubani na kutwanga maeneo mawili ya jeshi la Israel katika eneo Jaffa karibu na Tel Aviv na kusema kuwa hayo ni majibu ya moja kwa moja ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Yemen jana Ijumaa, operesheni hiyo ya kijeshi imeendeshwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani za "Yaffa" zilizotengenezwa na wataalamu wa Yemen ikiwa ni sehemu ya uungaji mkono thabiti kwa wananchi wa Palestina na wanamapambano wa Muqawama huko Ghaza.
Jana hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walifanya shambulio baya la anga kwenye kitongoji cha Shujaiya cha mji wa Ghaza na kuua shahidi takriban raia 29 — wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. Zaidi ya Wapalestina wengine 50 wamejeruhiwa na wengine kadhaa bado wamekwama chini ya vifusi.

Wizara ya Afya huko Ghaza imesema kuwa, tangu mauaji ya umati ya Israel yaanze mwezi Oktoba 2023, zaidi ya watu 50,912 wameshauawa shahidi na zaidi ya 115,688 kujeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza pekee.
Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimeendelea kusisitizia msimamo wao usiotetereka wa kusimama kidete pamoja na wananchi wa Palestina vikisema kuwa kamwe hawatajiondoa kwenye msimamo huo.
"Hatutoacha; na uchokozi wa Marekani dhidi ya Yemen hautotuzuia kutekeleza wajibu wetu wa kidini, kimaadili na wa kibinadamu kuhusu Ghaza hadi uvamizi huo utakapokoma na Ghaza kuachwa huru bila ya kuzingirwa," imesema taarifa ya jeshi la Yemen.